1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden azindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9

15 Januari 2021

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden ameuzindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9 kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona na kuufufua uchumi wa nchi hiyo.

Joe Biden US-Präsident
Picha: Susan Walsh/dpa/AP/picture alliance

Akizungumza Alhamisi usiku huko Wilmington Biden amesema masuala hayo mawili ni kipaumbele chake cha kwanza na kwamba chanjo ya virusi vya corona inapaswa kutolewa ili kuwaokoa mamilioni ya Wamarekani.

''Mpango wa kutoa chanjo nchini Marekani haujafanikiwa hadi sasa. Kesho nitatangaza mpango wetu wa chanjo na kufanya marekebisho ili kulifikia lengo letu la chanjo milioni 100 mwishoni mwa siku zangu 100 za mwanzo kama rais. Hii itakuwa moja ya changamoto ngumu zaidi ya kiutendaji ambayo tumewahi kufanya kama taifa,'' alisisitiza Biden.

Biden amesema Mpango wa Uokozi wa Marekani utashughulikia janga la COVID-19 pamoja na kutoka moja kwa moja msaada wa kifedha na misaada kwa Wamarekani ambao wana uhitahi zaidi.

Soma zaidi: Mpango wa uokozi wa dola Trilioni 1 wanukia Marekani 

Rais huyo mteule wa Marekani amesema mwezi ujao atakapoenda bungeni katika kikao cha pamoja cha Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti, kwa mara ya kwanza atawasilisha mpango wake wa kuijenga tena nchi kuwa bora. Amesema utakuwa uwekezaji wa kihistoria katika miundombinu, viwanda, uvumbuzi na utafiti na maendeleo ya nishati safi.

Muuguzi wa Marekani akichomwa chanjoPicha: Mark Lenninhan/AFP/Getty Images

Mapema wiki hii, serikali ya Rais Donald Trump ilitangaza kuwa itatoa dozi zote za chanjo zilizopo. Ilisema itayaagiza majimbo kuanza mara moja kutoa chanjo kwa kila Mmarekani mwenye umri wa miaka 65 na zaidi pamoja na mamilioni ya wazee wenye maradhi ambayo yanawaweka hatarini kufa kutokana na virusi vya corona. Zaidi ya watu 385,000 wamekufa kutokana na COVID-19 nchini Marekani.

Merkel ataka vizuizi zaidi

Ama kwa upande mwingine, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka hatua za haraka zaidi zichukuliwe kuzuia kusambaa kwa aina mpya ya virusi vya corona nchini humo.

Hayo ameyaeleza siku ya Alhamisi wakati wa mkutano na maafisa wa ngazi ya juu wa chama chake cha Christian Democratic Union, CDU.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel Picha: John MacDougall/AP/picture alliance

Merkel amepanga kukutana na viongozi wa majimbo yote 16 wiki ijayo kuzungumzia vizuizi hivyo. Taarifa zinaeleza kuwa mkutano huo unaweza kufanyika Jumatatu au Jumanne ijayo. Awali viongozi hao walikuwa wakutane Januari 25.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Ujerumani, Robert Koch, imerekodi visa vipya 25,164 vya COVID-19 na vifo vipya 1,244 na kuifanya idadi jumla ya vifo kufikia 43,881.

Mkuu wa taasisi ya Robert Koch, Lothar Wieler amesema vizuizi havitekelezwi ipasavyo kama ilivyokuwa wakati wa wimbi la kwanza la virusi vya corona. Wieler Amesema watu zaidi wanatakiwa kufanyia kazi nyumbani na kuongeza kuwa vizuizi vilivyopo vinahitaji kuimarishwa zaidi.

(AFP, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW