1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Harris watoa hotuba ya shukrani kwa ushindi

8 Novemba 2020

Rais mteule wa Marekani Biden na makamu wake, Kamala Harris, wametowa hotuba zao za kwanza za shukrani kufuatia ushindi wao kwenye uchaguzi uliokuwa na mchuano mkali, huku Trump akikataa kuyatambua matokeo hayo.

USA Wilmington | Rede Joe Biden und Kamala Harris nach dem Wahlsieg
Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Akizungumza kwenye uwanja wa Wilmington katika jimbo lake la Delaware, Biden aliwaambia maelfu ya wafuasi wake kwamba Wamarekani wamewapa yeye na Kamala Harris ushindi wa wazi ambao watautumia kurejesha kile alichokiita "roho ya Marekani."

Kwenye hotuba yake hiyo ya shukurani, Biden aliahidi kwamba atakuwa rais wa kuwaunganisha na sio kuwagawa, katika kile kinachoonekana kuupiga kijembe utawala wa mtangulizi wake, Donald Trump, ambaye kauli yake ya "Marekani Kwanza" inatajwa kuleta migawanyiko mikubwa ndani na nje ya Marekani. 

Akizungumza moja kwa moja na wapigakura wenye asili ya Afrika, ambao pamoja na Waislamu walimpigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali, Biden aliwaambia daima wamekuwa wakimuunga mkono kama naye anavyowaunga mkono. 

Harris awashukuru wanawake kwa kulinda demokrasia

Makamu wa rais mteule wa Marekani, Kamala Harris.Picha: Jim Watson/AFP/Getty Images

Kwa upande wake, makamu wa rais mteule, Kamala Harris, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza na pia Mmarekani wa kwanza mwenye asili za Afrika na Asia Kusini kushikilia nafasi hiyo nchini Marekani, alitumia hotuba yake ya shukurani kuwashukuru maelsu ya wanawake wa Kiafrika waliothibitisha kwamba "wao ndio uti wa mgongo wa demokrasia" ya Marekani. 

Kamala, ambaye ni mtoto wa wahamiaji kutokea Jamaica na India, alisema kwamba amepata fursa hiyo ikiwa ni miaka 100 tangu Mabadiliko ya 19 ya Kativa ya Marekani na miaka 55 tangu kusainiwa kwa Sheria ya Upigaji Kura, ambayo iliruhusu idadi ya Wamarekani wenye haki ya kuchaguwa na kuchaguliwa.

Alisema Biden amevunja kikwazo kikubwa ambacho kimekuwapo kwenye siasa za Marekani kwa kumchaguwa yeye kuwa mwanamke wa kwanza na pia mwenye mizizi ya wahamiaji wa Kiafrika na Kiasia kuwa makamu wake. 

Trump hajakubali kushindwa

Rais Donald Trump amekataa hadi sasa kukubali kushindwa.Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Mapema, vyombo kadhaa vya habari viliripoti kwamba Biden amechaguliwa kuwa rais wa 46 wa Marekani, baada ya matokeo ya jimbo la Pennsylvania kuupaisha ushindi wake wa kura maalum za wajumbe kutoka 254 hadi 290. 

Ushindi wa Biden dhidi ya Trump unahitimisha enzi iliyozigubika na kuzitia katika mtihani mkubwa siasa za Marekani. 

Hata hivyo, ushindi huo uliopokelewa vyema na ulimwengu unaiwacha Marekani ikiwa katika mpasuko na kugawika kuliko wakati wowote wa historia ya miongo kadhaa ya taifa hilo kubwa duniani.

Mwenyewe Trump ameapa kutokuyakubali matokeo hayo, akisema kuwa anaelekeza nguvu zake mahakamani kupinga kile alichokiita "wizi wa kura" uliofanywa na chama cha Democrat na kuungwa mkono na vyombo vya habari. 

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alikuwa mmoja miongoni mwa viongozi wa kwanza wa dunia kumpongeza Biden kwa ushindi wake, akisema anamtakia kila la kheri na ufanisi. Alimpongeza pia Kamala Harris kwa kuwa  "mwanamke wa kwanza kuchaguliwa makamu wa rais wa Marekani."

Reuters, AP