Biden kubadili mwelekeo wa mahusiano na Saudia
12 Oktoba 2022Rais Joe Biden ametoa tangazo hilo jana, siku moja baada ya seneta kutoka chama cha Democrats na mwenye ushawishi mkubwa Bob Menendez kusema Marekani inatakiwa kusitisha mara moja mahusiano na Saudi Arabia ikiwa ni pamoja na kuiuzia silaha. Menendez ni mwenyekiti wa kamati ya sera za kigeni ya bunge.
Kwenye mahojiano na kituo cha utangazaji cha Marekani cha CNN, Biden alisema kwa sasa hatazungumzia ni kitu gani wanachofikiria kukifanya.
Biden aondoka Saudi Arabia baada ya kukamilisha ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati kama Rais
Msemaji wa ikulu ya White House Karine Jean-Pierre amesema wataiangazia upya sera ya mahusiano baina ya mataifa hayo, ingawa hakueleza kwa kina juu ya namna mchakato huo utakavyoendeshwa na nani hasa atayeusimamia.
''Tunaangalia pale tulipo kwa sasa na tutafuatilia kwa karibu wiki na miezi inayokuja. Tutawasiliana na washirika wetu na wabunge. Na maamuzi yatafanywa mara baada ya kupitiwa kwa sera. Lakini huo ni mchakato tutakaochukua hapo baadae. Sina muda maalumu, lakini ni wazi hiki ni kitu tutakachokifuatilia kwa karibu. Na tumesema tangu mwanzo kwamba tunataka kuangazia upya na kuwa na mahusiano ya tofauti na Saudi Arabia na hasa baada ya uamuzi uliofanywa na OPEC+.'' alisema Jean-Pierre.
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan amesema uamuzi wa OPEC+ ulijikita kwenye misingi ya kiuchumi na ulifikiwa kwa pamoja na mataifa wanachama. Hata hivyo Marekani inapinga maelezo hayo.
Marekani inaituhumu Saudi Arabia kwa kula njama na Urusi ambayo inapinga ukomo wa bei ulioyowekwa na mataifa ya magharibi kwa mafuta kutoka Urusi, ambao ni sehemu ya mpango wa kuidhibiti Urusi baada ya kuivamia Ukraine.
Marekani yasema hawatapuuza kitisho cha Iran.
Maafisa wa Marekani wamekuwa wakijaribu kumshawishi mshirika wake mkubwa wa Arabuni, Saudi Arabia kuachana na wazo hilo la kupunguza uzalishaji, lakini mtawala wa taifa hilo mwana mfalme Mohammed bin Salman hakuonyesha kukubaliana nao.
Msemaji wa masuala ya usalama wa taifa katika ikulu ya White House John Kirby amesema Biden kwa kushirikiana na baraza la Congress wanatarajiwa kuangazia kwa pamoja namna ya kusonga mbele kimahusiano kati ya mataifa hayo mawili na kuongeza kuwa anaamini kwamba Biden ataona umuhimu wa kuanza mazungumzo kuhusu hilo mara moja.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Ned Price amesema siku ya Jumanne kwamba serikali ya Biden haitapuuza Iran ambayo ni mpinzani wake mkubwa na adui namba moja wa kikanda wa Saudi Arabia wakati watakapoiangazia sera hiyo.
Amesema kuna changamoto za kiusalama, na miongoni mwake zinatokea Iran. Na ndio maana hawataiweka pembeni kwenye majadiliano yao, kutokana na kitisho chake kwenye ukanda na nje ya mipaka ya ukanda huo.
Mashirika: RTRE