Biden kuishawishi NATO yupo thabiti katika uongozi
9 Julai 2024Ikulu ya Kremlin imesema inaufuatilia mkutano huo kwa karibu, huku China ikilaani kile ilichokiita kampeni ya jumuiya hiyo kuipaka matope Beijing kuhusiana na madai ya kuiunga mkono Urusi.
Rais Joe Biden anawakaribisha viongozi kutoka mataifa 32 wanachama wa muungano huo wa kijeshi kwa siku tatu kuanzia leo Jumanne, pamoja na viongozi wa Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, aliuambia mkutano wa habari kuelekea mkutano huo wa kilele wa mwaka wa 75, kwamba ushirikishwaji wa mataifa hayo yasio wanachama unadhihirisha kuwa usalama wao siyo wa kikanda, bali wa kimataifa.
Soma pia:Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka
Stoltengerg alisema hilo linadhihirika wazi katika vita nchini Ukraine, ambako Iran, Korea Kaskazini na China zinaunga mkono na kuwezesha kile alichokiita vita haramu vya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, kulingana na andiko la NATO.
Wizara ya mambo ya nje ya China imeukosoa muungano huo ulioasisiwa mwaka 1949 kutoa ulinzi wa pamoja dhidi ya uliokuwa Muungano wa Kisovieti, ambapo msemaji wake Lin Jian ameutaka kuacha kile alichokiita kampeni ya kuipaka China matope.
"Tunaihimiza NATO kurekebisha mtazamo wake potofu kuhusu China, kuachana na mawazo ya Vita Baridi na mchezo wa kutafuta ushindi."
Alielekeza ujumbe wake kwa NATO kwa kuongeza "kuachana na kuuza wasiwasi wa usalama, kuacha kuunda maadui wa kufikirika kila mahali, na kuacha kuunda vikundi vidogo kwa kisingizio cha ulinzi wa pande zote, na badala yake wafanye jambo linaloonekana kukuza amani ya ulimwengu, utulivu na maendeleo."
NATO yakutana katikati ya changamoto miongoni mwa washirika
Viongozi wa NATO wanakutana Washington chini ya kivuli cha vikwazo nchini Ukraine na chaguzi katika pande zote za kanda ya Atlantiki.
Biden anapambania maisha yake ya kisiasa baada ya kuboronga vibaya katika madahalo wa televisheni dhidi ya mpinzani wake na mkosoaji mkubwa wa NATO Donald Trump.
Nyota wa mkutano huo wa kiele anatazamiwa kuwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, anaetafuta ishara thabiti za uungwaji mkono licha ya ukweli kwamba NATO haitaipatia nchi yake mwaliko wa kujiunga na jumuiya hiyo.
Ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema itaufuatilia kwa karibu mkutano huo, kwasababu jumuiya hiyo imeitangaza Moscow kuwa adui na inataka kuishinda Urusi.
Soma pia:Viongozi wa NATO kujadili msaada zaidi kwa Ukraine
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, amewaambia waandishi habari kuwa Urusi inaichukulia NATO kuwa inayoshiriki kikamilifu katika mzozo wa nchini Ukraine.
Akizungumza kabla ya kuondoka kwenda kushiriki mkutano huo wa kilele, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameihakikishia tena Ukraine juu ya uungaji wake mkono wa muda mrefu katika vita na Urusi, wakati ambapo kwa upande mwingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizinyooshea kidole Ujerumani na Marekani kuwa wapinzani wakuu wa Ukraine kujiunga na NATO.