1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden kukutana na Xi katika mkutano wa APEC

13 Novemba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden, wiki hii atakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) utakaofanyika mjini San Francisco nchini Marekani

Rais wa China Xi Jinping (Kushoto) mwenzake wa Marekani Joe Biden( Katikati) na Vladimir Putin (Kulia)
Rais wa China Xi Jinping (Kushoto) mwenzake wa Marekani Joe Biden( Katikati) na Vladimir Putin (Kulia)Picha: Sergei Guneyev/Pool/picture alliance/Chip Somodevilla/Getty Images/Sergei Guneev/Sputnik/REUTERS

Viongozi mbali mbali wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa ushirikiano wa APEC, unaoyajumuisha mataifa wanachama 20, uliobuniwa miongo mitatu iliyopita katika enzi ambapo wabunge wa Marekani walishawishika kuwa biashara thabiti italeta pamoja Ukanda wa Pasifiki.

Washirika mbali mbali wa Marekani kuhudhuria mkutano wa APEC

Washirika wa Marekani watakaohudhuria mkutano hupo ni pamoja na waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese ambaye kwa muda wa mwezi mmoja uliopita amefanya ziara nchini Marekani na China, waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida na rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol.

Biden na Xi kukutana siku ya Jumatano

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani,  amesema kuwa Xi Jinping na Biden wanatarajiwa kukutana siku ya Jumatano pembezoni mwa mkutano huo wa APEC katika mkutano utakaolenga kuyaweka sawa mahusiano ambayo yamezorota kati ya mataifa hayo mawili lakini akaonya kutotarajiwa kwa matokeo makubwa.

Soma pia:Mazungumzo kati ya China na Marekani yameanza mjini San Francisco ambako mkutano huo wa kilele wa APEC unatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning, ameuambia mkutano wa kawaida wa waandishi wa habari kwamba viongozi hao wawili watazungumzia kwa kina kuhusu masuala ya kimkakati, ya jumla na ya mwelekeo kuhusu uhusiano wa China na Marekani,  pamoja na masuala makubwa yanayohusu maendeleo na amani duniani.

Mkutano kati ya Biden na Xi ni wa kwanza wa ana kwa ana tangu 2022

Mkutano huo kati ya Xi na Biden, unafuatia mfululizo wa mikutano katika miezi ya hivi karibuni kati ya viongozi wakuu wa China, Marekani na kwingineko  lakini utakuwa wa kwanza wa ana kwa ana kati ya viongozi hao wawili tangu mkutano wa Bali wa Novemba 2022.

Watu waandamana kupinga Jumuiya ya APECPicha: Carlos Barria/REUTERS

Marekani yajiepusha na Urusi

Tofauti na diplomasia yake inayolenga kuepusha mzozo na China, Marekani imejiepusha na Urusi, mwanachama wa ushirikiano huo wa APEC kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Soma pia: Trump ataka ushirikiano mpya kiuchumi na nchi za APEC

Rais wa Urusi Vladimir Putin, anayekabiliwa na waranti ya kukamtwa kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC hatarajiwi kamwe kuhudhuria mkutano huo wa San Francisco na Marekani imeweka hili wazi kwamba hajakaribishwa.

Badala yake, Urusi itawakilishwa na naibu waziri mkuu Alexei Overchuk, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu wa Urusi kuzuru Marekani tangu kuanza kwa vita vyake nchini Ukraine.

Mamia ya waandamanaji waandamana kuipinga Jumuiya ya APEC

Katika hatua nyingine, mamia ya waandamanaji wanaowajumuisha wale wanaopinga ubepari hadi wale wanayoiunga mkono Palestina, walikusanyika mjini San Francisco jana Jumapili mkesha wa mkutano huo wa APEC kuupinga ushirikiano huo.

Soma pia: China na Marekani wamekuwa katika mivutano ya muda mrefu na wamekuwa katika jitihada za kusuluhisha mivutano hiyo

Waandamanaji hao waliandamana mjini humo wakiwataka washiriki katika kongamano hilo la APEC kutoa kipaombele watu na sayari ya dunia badala ya kujikita katika biashara.

Mmoja wa waandamanaji hao Nik Evasco, ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba APEC ni aina ya serikali ya ukoloni mamboleo na kwamba wako hapo kuhakikihsa kuwa washirika wa kongamano hilo wanatoa kipaombele kwa  masuala yanayowaathiri watu na sayari ya dunia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW