1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kusitisha mauzo ya silaha UAE na Saudi Arabia

28 Januari 2021

Utawala wa Rais Joe Biden umesitisha kwa muda uuzaji wa silaha kwa mataifa ya Ghuba. Hatua hii inazuia mabilioni ya dola kwa mauzo ya silaha na kubadili maamuzi ya mwisho ya rais aliyeondoka madarakani Donald Trump.

Ukraine 2018 |  U.S. Air Force F-15 Kampfflugzeuge
Picha: Reuters/G. Garanich

Wizara ya mambo ya nje imesema itaikagua mikataba iliyotiwa saini na Trump kabla ya kuibatilisha au kuendelea nayo.

Utawala wa Biden leo Jumatano umetangaza kuwa utazuilia kwa muda mabilioni ya dola katika mauzo ya silaha kwa Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia. Waziri wa mambo ya Nje, Antony Blinken ameitaja hatua hiyo "kama ya kawaida kiutawala" akibainisha kuwa ilikuwa kawaida kwa utawala unaoingia madarakani kuipitia mikataba mikubwa ya silaha iliyoanzishwa na utawala uliomaliza muda wake.

Wizara hiyo imesema kusitisha kwa muda kutaruhusu utawala wa Biden kuhakikisha mauzo ya silaha za Marekani yanatimiza malengo ya kimkakati ya kujenga washirika wenye usalama, ushirikiano na uwezo.

Blinken katika siku yake ya kwanza ofisini leo Jumatano, amesema utawala mpya umeanzisha uchunguzi kamili wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi pia inachunguza maelezo ya mkataba wa amani wa Marekani na Taliban uliosainiwa karibu mwaka mmoja uliopita.

Antony Blinken Waziri wa mambo ya njePicha: REUTERS

Uamuzi wa kawaida

"Linapokuja suala la uuzaji wa silaha, ni kawaida mwanzoni mwa utawala kupitia mikataba yote, mauzo yoyote yanayosubiri ili kuhakikisha kuwa kile kinachozingatiwa ni jambo ambalo linaendeleza malengo yetu ya kimkakati na kuendeleza sera yetu ya kigeni. Kwa hiyo ndivyo tunavyofanya wakati huu." amesema Blinken.

Miongoni mwa mauzo ambayo yamesitishwa ni mpango mkubwa wa dola bilioni 23 wa kusambaza ndege 50 za kivita aina ya F-35 za kampuni ya Lockheed Martin kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu. Mkataba huo ulikubaliwa katika siku za mwisho za urais wa Trump, baada ya uchaguzi wa Novemba 6.

Benjamin Netanyahu, Donald Trump, Abdullah bin Zayed Al-NahyanPicha: Saul Loeb/AFP

Kufikia sasa bado haijulikani ni makubaliano yapi mengine yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya utawala wa Biden. Kama mgombea, Joe Biden aliahidi kusitisha uuzaji wa silaha kwa serikali ya Saudi Arabia katika juhudi za kusimamisha vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Irani huko Yemen.

Utawala wa Biden umesitisha au kukagua sera nyingi za kigeni zilizosainiwa na Trump, na kuelezea nia ya kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya 2015 na Iran, ambayo rais wa zamani Donald Trump alijiondoa, iwapo Iran itakubali kurudi katika makubaliano hayo.

Kusitisha kwa muda uuzaji wa silaha kwa Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, ambayo mkataba wake ulitiwa saini siku chache tu baada ya uchaguzi ambao pia unahusiana na Yemen, wakosoaji wanahofia kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia wanaweza kutumia silaha za viwango vya juu za Marekani kuendeleza vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na kusababisha athari kubwa kwa raia.

AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW