Biden kuzungumza na Rais Xi kuhusu puto la ujasusi
17 Februari 2023Katika maelezo yake ya kina aliyoyatoa jana juu ya sakata la Puto la China pamoja na vitu vitatu visivyojulikana ambavyo vilidunguliwa na ndege za kijeshi za Marekani, Rais Joe Biden hakusema ni lini atazungumza na Xi, lakini ameongeza kuwa Washington inaendelea kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na China juu ya suala hilo.China yasema Marekani imewahi kupeperusha maputo zaidi ya 10 katika anga yake
Wakati akisisitiza kwamba Marekani "haitafuti kuanzisha upya vita baridi" Biden amenukuliwa akisema kwamba hawezi kuomba radhi kwa kudungua puto hilo. Marekani imekuwa katika hali ya tahadhari tangu Puto hilo kubwa la China lilipoonekana kufuatilia safu ya maeneo nyeti ya silaha za nyuklia, kabla ya kudunguliwa nje ya pwani ya mashariki.
Aidha Biden ameongeza kuwa idara za kijasusi bado zinaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa vitu vitatu ambavyo havikutambulika na pia kudunguliwa kutokana na kutoa kitisho kwa usafiri wa anga. Kifaa cha kwanza kiliangushwa huko Alaska, kingine Canada na cha tatu kilitumbukia katika Ziwa Huron.
"Ndio maana nimeagiza timu yangu iniletee sheria kali zaidi za jinsi tutakavyoshughulikia vitu hivi visivyojulikana, kutofautisha kati ya vile ambavyo vina uwezekano wa kuleta hatari za kiusalama ambazo zinahitaji hatua na zile ambazo hazifanyi kazi. Lakini usifanye makosa! ikiwa kitu chochote kitaleta tishio kwa usalama wa watu wa Marekani, nitakidungua," alisema Biden.
Katika taarifa yake Biden amesema hakuna chochote kwa hivi sasa kinachoonyesha kwamba vifaa hivyo vitatu vinahusiana na mpango wa Puto la kijasusi la China. Idara za kijasusi za Marekani zinaamini kwamba vitu hivyo vina uwezekano kuwa vya kampuni binafsi, burudani au taasisi za utafiti.
China inadai kuwa puto hilo lenye ukubwa wa futi 60 lilikuwa likifuatilia hali ya hewa, lakini Marekani inasema kuwa ni wazi lilikuwa puto la kijasusi. Biden ambaye hakulizungumzia kwa undani suala hilo tangu litokee amelazimika kuvunja ukimya baada ya wabunge kushikiniza maelezo ya kina juu ya tukio hilo ambalo limewashangaza Wamarekani wengi.Marekani yaliona puto la pili la ujasusi la China
Gazeti la Washington Post liliripoti siku ya Jumanne kwamba jeshi la Marekani na mashirika ya kijasusi yalifuatilia puto hilo tangu lilipopaa kutoka mkoa wa kisiwa cha Hainan, kusini mwa China na kudunguliwa kwenye pwani ya Carolina Kusini. Wabunge wa Marekani wamekosoa utawala wa Biden kuruhusu puto hilo kuruka anga yake ikiwa ni pamoja na karibu na vituo nyeti vya kijeshi.
Tukio hilo limeongeza mtafaruku wa kidiplomasia, baina ya China na Marekani huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akielekea mjini Munich katika mkutano wa usalama. Duru zinasema kwamba Blinken huenda akatumia fursa hiyo kukutana na mwenzake wa China Wang Yi ambaye pia anahudhuria mkutano huo.