1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Mgogoro wa kisiasa Marekani watishia msaada kwa Kyiv

5 Oktoba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amedhihirisha wasiwasi wake kuwa mgogoro wa kisiasa unaoendelea huko Washington, unaweza kuuweka mashakani msaada wa taifa hilo kwa Ukraine.

Litauen | Nato-Gipfel in Vilnius | US-Präsident Joe Biden und Wolodymyr Selenskyi
Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP/Getty Images

Katika muda wa takriban mwezi mmoja na nusu, Bunge la Marekani linatarajiwa kuidhinisha bajeti ya mwaka ujao ambayo Ikulu ya White House inatarajia kuwa itajumuisha pia msaada mpya kwa Ukraine wa dola bilioni 24.

Ofisi ya rais Biden imesema fedha hizo ndizo zinazohitajika ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Ukraine kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Hata hivyo, utawala wa Biden unakabiliwa na tatizo kubwa kwa kuwa Wabunge wa mrengo mkali wa kulia wanapinga vikali msaada huo kwa Ukraine, jambo lililochangia pia kuondolewa katika wadhifa wake, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Kevin McCarthy.

Soma pia: Kevin McCarthy aondolewa kama Spika wa Bunge la Marekani

Aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Kevin McCarthyPicha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

Alipoulizwa kuhusu athari za kuondolewa kwa Kevin McCarthy na msaada kwa Kyiv, Rais Biden amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano kuwa jambo hilo linamtia wasiwasi.

"Lakini ninafahamu kwamba kuna wabunge wengi waliochaguliwa katika Baraza la Wawakilishi na katika Baraza la Seneti, kutoka pande zote mbili, ambao wanaunga mkono msaada wa ufadhili kwa Ukraine," aliongeza Biden.

Biden: Ushindi wa Ukraine ni kwa maslahi ya Marekani

Biden amesisitiza kuwa ushindi wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi, ni kwa maslahi ya Marekani na washirika wake.

Siku ya Alhamisi, Biden atakutana na washauri wake wa karibu wanaohusika na masuala ya usalama wa taifa akiwemo mkuu mpya wa majeshi, ili kujadili miongoni mwa mambo mengine, suala hili la msaada kwa Ukraine.

Biden ameahidi kutoa hotuba itakayosisitiza  umuhimu wa msaada wa kifedha na kijeshi kwa Kiev,  katika dhamira ya kutafuta uungwaji mkono wa wabunge wengi. "Ni muhimu kwa Marekani na washirika wetu kutimiza ahadi zetu," amesema Biden.

Rais wa Marekani Joe Biden (katikati) akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza lake la Mawaziri: Washington 02.10.2023Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo rais huyo wa Marekani anafahamu ni jinsi gani Baraza la Congress lakini pia maoni ya umma nchini Marekani yalivyochoshwa na misaada hiyo kwa Ukraine.

Soma pia: Tishio la Marekani kusimamisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Joe Biden amesema Washington ilizileta pamoja nchi zaidi ya 50 ili kuisaidia Ukraine na kwamba kwa sasa wanao uwezo wa kufadhili "msaada ujao" akisisitiza kuwa zipo "njia zingine" za kupata pesa, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Taasisi ya Ujerumani ya Kiel inayojikita katika Uchumi wa Dunia na inayofuatilia misaada inayotolewa kwa Ukraine, imebainisha kuwa msaada wa Marekani kwa Ukraine umefikia takriban dola bilioni 75, ikiwa ni pamoja na zaidi ya dola bilioni 42 za msaada wa kijeshi. Hii inaifanya Marekani kuwa mchangiaji mkubwa zaidi duniani kwa taifa hilo.

(AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW