1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin wakutana kwa mara ya kwanza

16 Juni 2021

Viongozi wote wanataraji mazungumzo yao yatakwenda vizuri

Schweiz Genf | Gipfeltreffen Biden und Putin
Picha: Denis Balibouse/Reuters/AP/picture alliance

Mkutano uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kati ya rais Joe Biden wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi unaendelea baada ya kufunguliwa mchana wa leo,huko Geneva nchini Uswisi. Viongozi hao wawili baada ya kuwasili kwenye eneo la mkutano walikaribishwa na mwenyeji wao rais wa Uswisi Guy Parmelin.

''Kwa niaba ya serikali ya Uswisi nawakaribisha nyote rais wa shirikisho la Urusi na rais wa Marekani hapa Geneva,mji wa amani. Tunafuraha kwa kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kilele wa amani kutokana na utamaduni wetu wa kufadhili mikutano ya maridhiano na maelewano. Nawatakia nyote mazungumzo mazuri kwa maslahi ya nchi zote mbili na ulimwengu mzima kwa ujumla.''

Mkutano huo unatarajiwa kugubikwa zaidi na hali ya kutokubaliana katika masuala mengi na matarijio ya kupatikana suluhu yakiwa madogo mno. Ni mkutano wa kwanza kabisa wa kilele kati ya marais hao wa Marekani na Urusi tangu alipoingia madarakani rais Biden.

Picha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

Kwenye duru ya kwanza Rais Joe Biden alikuwa pamoja na waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken wakati rais Putin nae akiongozana na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov na wakalimani kadhaa. Mkutano mkubwa zaidi utakaofunga mazungumzo ya viongozi hao utahudhuriwa na wajumbe wengi,kwa upande wa Marekani atashiriki waziri wa mambo ya nje Anthony Blinken,mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan,naibu waziri wa mambo ya nje anayehusika na masuala ya kisiasa Victoria Nuland,balozi wa Marekani nchini Urusi John Sulivan miongoni mwa wengine huku upande wa Urusi nao akiwepo waziri Lavrov,na naibu wake Sergei Ryabkov,mshauri wa mambo ya nje wa rais Putin Yuri Ushakov,mkuu wa majeshi Urusi jenerali Valery Gerasimov,balozi wa Urusi,mjini Washinton Anatoly Antonov miongoni mwa wengine.

Watakuwepo pia wajumbe wa Urusi kuhusu Ukraine na Syria na msemaji wa Putin Dmitry Peskov.

Viongozi wote wawili kabla ya kuanza kikao chao walisema wanataraji mazungumzo yao yanaweza kuwaelekeza kwenye uhusiano wa uthabiti zaidi na wakueleweka japokuwa wote wanavutana kuhusu kila kitu. Kuanzia suala la udhibiti wa silaha na udukuzi wa kimtandao mpaka kwenye suala la kuingiliwa uchaguzi na Ukraine.

Picha: Peter Klauzner/AFP

Wakati wakiingia kwenye eneo la mkutano Rais Biden aliuita mkutano huo kuwa ni mazungumzo kati mbili zenye nguvu kubwa na akaongeza kusema kwamba siku zote ni bora kukutana ana kwa ana.Na rais Putin upande wake akasema anataraji mazungumzo hayo yatakuwa na tija. Lakini pia rais Putin aliweka mkazo kwamba kuna masuali mengi kuhusu uhusiano kati ya Urusi na Marekani ambayo yanahitaji mazungumzo ya ngazi za juu kabisa.

Mwanzoni kabisa walipokutana viongozi hao kabla ya kuingia kikaoni,ilizuka hali ya hekaheka ya waandishi habari kuuliza maswali chungunzima  kwa fujo na moja ya swali,aliulizwa rais Biden ikiwa anamuamini Putin,rais huyo wa Marekani alitikisa kichwa.

Lakini muda mfupi baadae mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu akatoa taarifa mara moja iliyosema kwamba tukio hilo la rais Biden kutikisa kichwa halikuwa na maana ya kuashiria anamuamini mwenzake wa Urusi Vladmir Putin.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW