1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden na Trump kukutana Whitehouse

Angela Mdungu
13 Novemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden wa Chama cha Democratic anatarajiwa kumkaribisha mshindi wa Urais kwa tiketi ya Republican Donald Trump katika Ikulu ya Marekani, ishara ya kuanza kwa makabidhiano ya mamlaka kwa njia ya amani.

Trump na Biden walipokutana kwenye mjadala wa Urais mwezi Juni
Rais mteule Donald Trump na Rais Joe Biden Picha: Artem Priakhin/Sipa/Sopa/picture alliance

Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre amesema mkutano wa Rais mteule Donald Trump na Biden umedhamiria kuhakikisha kuwa makabidhiano hayo ya mamlaka yanakwenda vizuri kabla ya kuapishwa kwa Trump mwezi Januari.

Jean Pierre amesema kuwa, "Kwa kweli linapokuja suala la ni kwanini Rais Biden anafanya hivi, ni kwasababu anaamini katika kufuata kanuni. Anaamini katika taasisi yetu. Anaamini katika makabidhiano ya amani ya madaraka. Mlimsikia akizungumza hili wiki iliyopita, siku mbili baada ya watu wa Marekani kufanya uamuzi katika uchaguzi huu."

Soma zaidi: Biden amualika Trump katika Ikulu ya White House

Rais Biden pia atatumia mwaliko wake kwa Trump kumpongeza kwa ushindi wake. Licha ya wanachama wa Democratic kumtaja Trump kama kitisho kwa demokrasia,  Biden ameendelea kufuata taratibu za makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani.

Itakumbukwa kuwa Trump, alikwepa kufuata taratibu hizo aliposhindwa katika uchaguzi uliomweka Biden madarakani mwaka 2020.

Kabla ya kukutana na Rais Biden, Trump anapanga kukutana na viongozi wa juu wa wa bunge la Marekani. Chama chake kinatarajiwa kudhibiti baraza la seneti na Baraza la wawakilishi mara tu bunge jipya litakapokutana mwezi Januari.

Mkutano huo ni moja kati ya matukio machache yaliyowahi kuwakutanisha wawili hao. Mnamo mwezi Juni walikutana mwishoni mwa mjadala wa wagombea Urais uliorushwa kwa njia ya televisheni, muda mfupi kabla ya Biden kujitoa katika kinyang'anyiro hicho. Walionana tena katika kumbukumbu ya Septemba 11 jijini New York licha ya kuwa hakukuwa na mazungumzo yoyote kati yao.

Rais mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Trump amteua Elon Musk na Ramaswamy kuhakikisha ufanisi wa serikali

Katika hatua nyingine, Rais mteule wa Marekani Donald Trumpamewataja bilionea Elon Musk na aliyewahi kuwa mgombea urais wa chama cha Republican Vivek Ramaswamy kuongoza idara mpya ya ufanisi wa serikali katika uongozi wake.

Trump amesema Musk na Ramaswamy wataweka msingi kwa utawala wake kuondokana na urasimu wa serikali. Idara yao itaondoa pia kanuni zisizo na ulazima, kuondoa matumizi yasiyo ya msingi na kuunda upya mashirika ya serikali.

Kulingana na taarifa hiyo, idara hiyo mpya itafanikisha kutimia kwa ndoto za muda mrefu za chama cha Republican na kutoa ushauri na mwongozo nje ya serikali. Trump ameashiria kuwa majukumu ya Musk na Ramaswamy  si rasmi na hayatahitaji kupitishwa na seneti hali itakayomruhusu Musk kuendelea kuwa mkuu wa kampuni ya Tesla, Jukwaa la X na Kampuni ya roketi ya Space X.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW