1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Biden na Xi wakubaliana kuimarisha mahusiano yao

16 Novemba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi jinping, wamekubaliana katika mkutano wao wa kwanza ndani ya mwaka mmoja, kurejesha mawasiliano yao ya kijeshi licha ya Biden kumuita Xi Dikteta.

Joe Biden wa Marekani na Xi Jinping wa China
Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi JinpingPicha: Doug Mills/AP Photo/picture alliance

Viongozi hao wawili wa Marekani na China walipeana mikono na kutembea pamoja katika bustani moja ya kihistoria wakati wa mazungumzo yao yaliyochukua masaa manne, yaliokuwa na lengo la kupunguza mivutano inayoendelea kukua kati ya mataifa hayo mawili makubwa kiuchumi na kuyazuia pia kuingia katika mgogoro kamili.

Biden na Xi pia, walikubaliana kudhibiti uzalishaji wa dawa ya fentanyl, inayotumika kama dawa ya kulevya inayoleta madhara makubwa Marekani. Xi amesema anawahurumia waathiriwa wa dawa hiyo iliyosababisha janga nchini humo.

Biden na Xi wakubaliana kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano

"Napenda mfahamu kwamba China ninawahurumia sana watu wa Marekani, hasa vijana wanaosumbuliwa na fentanyl. Rais Biden na mimi tulikubaliana kuanzisha kikundi kazi kuhusu udhibiti wa mihadarati, kuendeleza ushirikiano wetu ili kuisaidia Marekani kukabiliana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya," alisema Xi.

Licha ya hayo, viongozi hao wawili wameendelea kutofautiana kuhusu suala la Taiwan ambapo Xi alimuelezea mwenzake wa Marekani kuacha kutoa silaha kwa kisiwa hicho na kwamba suala la kuiunganisha Taiwan na China haliwezi kuzuilika. China inadai kisiwa hicho kinachojitawala chenyewe kuwa sehemu yake na haijaondoa uwezekani wa kukirejesha kwa nguvu.

China yasema tamko la Biden halikubaliki

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa China Mao Ning Picha: Kyodo/picture alliance

Biden aliuambia mkutano wa waandishi habari kwamba mazungumzo yake na Xi, aliyemfahamu tangu mwaka 2011 yalikuwa ya kujenga na yenye tija. Katika mkutano huo mwaandishi mmoja aliuliza iwapo Biden anamuona Xi kama dikteta kama alivyosema miezi kadhaa ya nyuma na Biden akajibu kwamba ndio, bado ni dikteta. Licha ya matamshi hayo Xi alisema China iko tayari kuwa mshirika na rafiki wa Marekani.

Biden na Xi watarajiwa kujadili namna ya kuyarekebisha mahusiano ya nchi zao

Baada ya tukio hilo, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa China Mao Ning amesema matamshi ya Biden ni kosa, hayakubaliki na China inayapinga vikali. Amesema tamko kama hilo ni baya na linaonyesha ubabe wa kisiasa. Ning ameongeza kuwa watu hawana nia njema na wanajaribu kuharibu uhusiano wa China na Marekani akisema hilo halitafaulu. Lakini hakutoa maelezo zaidi ya ni nani hasa aliyekuwa anamzungumzia.

Mkutano wa marais wa Marekani na China una maana gani kwa Ujerumani

Kingine kilichojadiliwa katika mkutano wa Joe Biden na Xi Jinping ni vita vya Israel na Hamas na pia vita vya Ukraine ambapo nchi zao zimejikuta zikiunga mkono pande tofauti za mzozo huo.

Mara ya mwisho kwa rais Joe Biden na mwenzake Xi Jinping kukutana ni Novemba mwaka jana walipofanya mazungumzo mjini Bali Indonesia. Uhusiano wao ulizidi kuingia doa baada ya Marekani Kulidungua puto la kijasusi lililoonekana katika anga yake mwezi Februari mwaka huu.

afp/dpa/reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW