1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Biden: Operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza imepitiliza

9 Februari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden, amesema operesheni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza kujibu shambulizi la Hamas la Oktoba 7 imepitiliza na inapaswa kusitishwa

Rais wa Marekani Joe Biden akitoa hotuba katika ikulu ya White House ya Marekani mnamo Februari 8, 2024
Rais wa Marekani Joe Biden Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Akiwahutubia wanahabari katika ikulu ya White House ya Marekani, Biden amekiri kuwa hatua za jeshi la Israel kuelekea Ukanda wa Gaza sasa zinapaswa kukomeshwa.

Akizungumzia msaada wa kibinadamu katika eneo hilo laGaza lililozingirwa, Biden amesema kuwa awali, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi, hakutaka kufungua mpaka wake ili kuruhusu msaada huo kuingizwa katika ukanda huo lakini akamshawishi kufanya hivyo.

Biden asema watu wasiokuwa na hatia wanateseka Gaza

Biden pia amesema kuwa kuna watu wengi wasiokuwa na hatia wanaokufa kwa njaa, wanaopata shida, na pia kufa na kuongeza kuwa hali hiyo haina budi kukomeshwa.

Soma pia: Blinken aondoka Mashariki ya Kati bila mafanikio

Uungaji mkono wa Marekani kwa vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas, umesababisha mashambulizi mengi dhidi ya wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo, pamoja na ukosoaji wa utawala wa Biden ndani na nje ya nchi.

Raia wa Palestina waomboleza jamaa zao waliofariki mjini RafahPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Katika hatua nyingine msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, amesema jana kwamba nchi hiyo haiungi mkono operesheni ya kijeshi yaIsraelkatika mji wa Rafah, Kusini mwa Gaza.

Jeshi la Israel liliongeza mashambulizi yake ya anga dhidi ya Rafah hapo jana, huku mashuhuda wakiripoti kufanywa kwa mashambulizi zaidi ya usiku kucha.

Watu 100 wauawa katika shambulizi la Rafah

Mapema leo, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, imesema kuwa zaidi ya watu 100 waliuawa katika saa za usiku. Wakati huohuo, Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema kuwa watoto watatu wamefariki katika mashambulizi hayo ya Rafah.

Soma pia:Blinken yuko Misri kutafuta suluhu ya mzozo wa Gaza

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema habari za kuingiliwa kwa mji huo wa Rafah ni za kushtusha na kuonya kuwa hatua hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa janga la kibinadamu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW