1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Starmer kujadili silaha za masafa marefu kwa Ukraine

13 Septemba 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais Joe Biden watajadili Ijumaa ombi la Kyiv kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi, katika mkutano wao mjini Washington, unaoweza kuwa wa mwisho kabla ya uchaguzi.

USA | Mkutano wa Kilele wa NATO | Keir Starmer na Joe Biden
Starmer na Biden walikutana kwa mara ya kwanza katika mkutano wa NATO Julai 10, 2024.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Kyiv inazishinikiza Washington na London kuondoa kizuizi kuhusu matumizi ya silaha zilizotengenezwa na mataifa hayo mawili kushambulia ndani kabisaa ya Urusi, huku Rais wa Urusi Vladimir Putin akionya kwamba kuipatia Ukraine ruhusa kama hiyo kutamaanisha NATO "iko vitani" na Moscow.

Vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa Biden, ambaye anahofia kuchochea mzozo wa nyuklia, alikuwa tayari kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya Uingereza na Ufaransa yanayotumia teknolojia ya Marekani lakini si makombora yaliyotengenezwa na Marekani yenyewe.

Mazungumzo hayo yanakuja wakati ambapo Biden yuko njiani kuondoka madarakani na uchaguzi wa Marekani wa Novemba mwaka huu ni mchuano kati ya Mdemokrat Kamala Harris na Donald Trump wa Republican.

Trump alikataa mara kwa mara kuunga mkono upande wowote kwenye vita hivyo wakati wa mjadala na Harris siku ya Jumanne, akisema tu: "Nataka vita kumalizika."

Starmer anatazamiwa kukutana na Biden katika Ofisi ya Oval saa 10:30 jioni kwa saa za Washington, lakini hana mikutano iliyoratibiwa kwa wakati huu na Trump au Harris, ambao wote watakuwa kwenye kampeni siku ya Ijumaa.

Starmer na Biden wakiwa kwenye mkutano wa kilele wa jumuiya ya NATO mjini Washington, Julai 10, 2024.Picha: Nathan Howard/REUTERS

"Hii ni mikutano ya kimkakati ya kujadili Ukraine na kujadili Mashariki ya Kati, na kwa hivyo itakuwa katika kiwango hicho cha majadiliano ya kimkakati ambayo tutashiriki kesho na rais," Starmer alisema Alhamisi.

Soma pia: US, UK kutafakari ombi la Kyiv kulegeza vikwazo vya kutumia silaha zao ndani ya Urusi

Ziara yake, ambayo ni ya pili Washington tangu chama chake cha Labour kiliposhinda uchaguzi mnamo Julai baada ya miaka 14 -- pia inalenga kuzungumzia tofauti juu ya vita vya Gaza.

Wiki iliyopita, serikali ya Starmer ilitangaza vizuwizi kwa baadhi ya silaha kwa Israel, ikielezea wasiwasi kuwa zinaweza kutumika kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ikulu ya White House imekataa kukosoa uamuzi huo wa Uingereza, lakini jarida la Politico liliripoti kuwa Washington iliiuliza London kitaifanya kubadilisha uamuzi wake -- ambapo jibu lilikuwa usitishaji vita Gaza.

Kushughulikia matakwa ya Ukraine

Lakini Ukraine ndiyo itakayoangaziwa zaidi, huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu hasara inayoikabili kwenye uwanja wa vita zaidi ya miaka miwili na nusu tangu kuanza kwa vita hivyo vya uvamizi wa Urusi.

Biden alisema Jumanne kwamba "anafanyia kazi" matakwa ya Ukraine, wakati wanadiplomasia wakuu wa Marekani na Uingereza Antony Blinken na David Lammy walipofanya ziara ya nadra ya pamoja mjini Kyiv siku ya Jumatano.

Blinken aliahidi kwamba Washington sasa ingepitia kwa haraka ombi la muda mrefu la Kyiv na "itarekebisha, tutarekebisha inavyohitajika" ili kuisaidia Ukraine kujilinda.

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

04:33

This browser does not support the video element.

Washington kwa sasa inaruhusu Ukraine kulenga tu shabaha za Urusi katika maeneo yanayokaliwa ya Ukraine na baadhi katika maeneo ya mpaka wa Urusi yanayohusiana moja kwa moja na operesheni za kivita za Moscow.

Soma pia:EU, Marekani: Tutachukua hatua iwapo Iran inapeleka makombora Urusi 

Lakini Putin, ambaye ametahadharisha kuhusu mgogoro wa nyuklia tangu kuanza kwa uvamizi wake wa Februari 2022 nchini Ukraine, alizionya Marekani na Uingereza dhidi ya hatua hiyo.

"Hii ingebadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya mzozo huo. Itamaanisha kuwa nchi za NATO, Marekani, nchi za Ulaya, ziko vitani na Urusi," alisema siku ya Alhamisi.

Biden ameiunga mkono Ukraine kwa nguvu tangu uvamizi wa Urusi na kuipatia ufadhili wa mabilioni ya dola kama msaada na mtaji wa kisiasa nyumbani. Lakini amekuwa akisita kutoa silaha nzito -- huku Ukraine ikilazimika kusubiri hadi mwaka huu kupata ndege za F-16.

Donald Trump amekuwa tepetepe katika kuonyesha uungwaji mkono kwa Kyiv, na mara kwa mara amemsifu Putin.

Katika mdahalo wake na Harris siku ya Jumanne, aliahidi kupata makubaliano ya kumaliza vita "kabla hata sijawa rais" -- makubaliano ambayo Waukreni wengi wanahofia yatawalazimu kukubali kuachia maeneo yaliotekwa na Urusi.

Makamu wa Rais Harris kwa upande wake ameahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine iwapo atachaguliwa.     

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW