1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Starmer waahirisha uamuzi wa makombora ya Ukraine

14 Septemba 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais wa Marekani Joe Biden Ijumaa waliahirisha uamuzi wa kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na nchi za Magharibi kuishambulia Urusi.

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu Keir Starmer mjini Washington
Rais Joe Biden akikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer katika Ikulu ya White House mjini Washington, Marekani, Septemba 13, 2024.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Katika mkutano wao uliofanyika ikulu ya White House jana Ijumaa, Waziri Mkuu Starmer alizungumzia namna Uingereza na Marekani zinavyofungamana kimkakati katika majaribio yao ya kutatua mzozo wa Ukraine.

Starmer alisema wiki na miezi inayokuja itakuwa muhimu nchini Ukraine, na kuongeza kuwa itakuwa muhimu kwa mataifa hayo mawili kuendelea kuisadia nchi hiyo ya Ulaya Mashariki katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Hata hivyo viongozi hao wamechelea uamuzi wa kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu yaliotolewa na mataifa ya magharibi kushabulia ndani ya Urusi, mpango ambao uliibua vitisho vikali kutoka Moscow juu ya vita na jumuiya ya NATO.

Starmer aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba alikuwa na "majadiliano mapana kuhusu mkakati" na Biden lakini kwamba "haukuwa mkutano kuhusu uwezo makhsusi."

Soma pia:US, UK kutafakari ombi la Kyiv kulegeza vikwazo vya kutumia silaha zao ndani ya Urusi

Lakini kiongozi huyo wa chama cha Labour ameashiria kwamba yeye na Biden sasa watajadili mpango huo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York wiki moja baada ya ijayo "na kundi kubwa la watu binafsi."

Kombora la masafa amrefu la Storm Shadow ambalo Ukraine inataka idhini a kutumia dhidi ya Urusi.Picha: Lewis Joly/AP/picture alliance

Kabla ya mkutano huo maafisa walikuwa wamesema Starmer angemshinikiza Biden kuunga mkono mpango wake wa kutuma makombora ya Uingereza chapa ya Storm Shadow nchini Ukraine ili kupiga ndani zaidi ndani ya Urusi mnamo wakati washirika wakizidi kuwa na wasiwasi kuhusu hali katika uwanja wa vita.

Katika mkutano huo Biden alipuuza onyo la Rais wa Urusi Vladimir Putin kwamba kuruhusu Ukraine kurusha makombora ya masafa marefu kunamaanisha nchi za Magharibi "zilikuwa vitani" na Urusi.

Biden: Simfikirii Vladmir Putin

Alipoulizwa na waandishi habari kuhusu onoy hilo la Putin, Rais Biden alisema hafikirii sana kuhusu Putin. Biden pia alimshukuru Starmer kwa mchango wa Uingereza katika kuisadia Ukraine, na kusema watu wa Ukraine watashinda dhidi ya Putin.

Lakini wakati Biden akisema ni "wazi kwamba Putin hatashinda katika vita hivi," anasita kuidhinisha matakwa ya Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya ATACMS kushambulia ardhi ya Urusi.

Maafisa wa Marekani wanaamini kuwa makombora hayo hayataleta mabadiliko makubwa katika kampeni ya Ukraine na pia wanataka kuhakikisha kuwa hifadhi ya Washington ya silaha hizo haimaliziki.

Soma pia: Biden, Starmer kujadili silaha za masafa marefu kwa Ukraine

Viongozi hao wawili walisema pia walijadili kuhusu vita vya Gaza, wakati ambapo Uingereza imesitisha baadhi ya vibali vya kusafirisha silaha kwa Israel kutokana na wasiwasi kwamba zinaweza kutumika kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

Kombora la ATAMCSPicha: DW

Taarifa ya ikulu ya White House ilisema Biden na Starmer walikubaliana juu ya "dhamira yao" kwa Israeli -- lakini walisisitiza "haja ya haraka" ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita na "haja ya Israeli kufanya zaidi kulinda raia" huko Gaza.

Awali Ikulu ya White House ilikuwa imepunguza uwezekano wa uamuzi kuhusu ombi la Ukraine kutokana na ziara ya Starmer, ya pili ya kiongozi huyo wa chama cha Labour katika Ikulu ya White House tangu aingie madarakani Julai.

Zelenskiy azidi kushinikiza

Hata hivyo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwashinikiza washirika wa Kyiv wa Magharibi kufanya zaidi.

Akizungumza mjini Kyiv, Zelensky alizishutumu nchi za Magharibi kwa "kuogopa" hata kuisaidia Ukraine kudungua makombora yanayorushwa kama zilivyofanya kwa Israel.

Zelensky aliongeza kuwa atakutana na Biden "mwezi huu" kuwasilisha "mpango wake wa ushindi" wa jinsi ya kumaliza miaka miwili na nusu ya vita na Urusi.

Urusi imeitikia kwa hasira kuhusu matarajio ya nchi za Magharibi kutoa silaha za masafa marefu kwa nchi iliyoivamia Februari 2022.

Soma pia:Urusi yaishambulia Ukraine kwa droni usiku kucha 

Katika ishara nyingine ya kuongezeka kwa mvutano, Urusi ilibatilisha nyaraka za wanadiplomasia sita wa Uingereza ambao iliwatuhumu kufanya ujasusi katika kile ambacho London imekiita madai "yasiyo na msingi".

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alionya kwamba kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za masafa marefu kutaitumbukiza NATO katika "vita vya moja kwa moja na... dola la nyuklia."

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Matokeo ya uchaguzi wa Marekani

Washirika wa Ukraine na Marekani wote kwa sasa wanasubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani utakaofanyika mwezi Novemba ambao unaweza kubadili sera ya Washington kuelekea Ukraine.

Biden yuko njiani kuondoka madarakani huku uchaguzi ukiwa na mchuano kati ya mrithi wake wa kisiasa wa chama cha Democratic Kamala Harris na rais wa zamani wa chama cha Republican Donald Trump.

Trump amekuwa akimsifu Putin mara kwa mara, na kukataa kuunga mkono upande wowote wa vita wakati wa mjadala na Harris siku ya Jumanne, akisema tu: "Nataka vita kukoma."

Starmer amekanusha kuwa na wasiwasi kuhusu urais wa Trump, na amesema haja ya kuisaidia Ukraine katika wiki na miezi ijayo ilikuwa ya dharura "bila kujali ratiba zinazoendelea katika mataifa mengine."

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW