1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Trump wakabiliana katika mdahalo wa uchaguzi wa rais

28 Juni 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na mpinzani wake Donald Trump wamekabiliana katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais unaopangwa Novemba mwaka huu. Kila mgombea alitafuta kumpiku mwenzake katika mbio za White House.

Mdahalo wa uchaguzi wa rais Marekani 2024
Biden na Trump walikabiliana katika mdahalo kwenye makao makuu ya CNN mjini AtlantaPicha: Justin Sullivan/Getty Images

Biden mwenye umri wa miaka 81, na Trump mwenye umri wa miaka 78, hawakusalimiana kwa kupeana mikono wakati waliposimama jukwaani katika studio za makao makuu ya televisheni ya CNN mjini Atlanta. Hakukuwa na watazamaji ukumbuni na vipaza sauti vilizimwa wakati kila mmoja akizungumza.

Soma pia: Mamilioni ya Wamarekani kufuatilia mdahalo wa Televisheni kati ya Joe Biden na Donald Trump

Biden alifungua mdahalo kwa kumlaumu Trump kwa "Uchumi ambao ulikuwa unaporomoka kwa kasi" wakati alipochukua usukani na janga ambalo "lilishughulikiwa vibaya mno, watu wengi walikuwa wanakufa."

Trump alijibu kwa kuishambulia rekodi ya utawala wa Biden. "Hajafanya kazi nzuri. Amefanya kazi mbaya. Na mfumuko wa bei unaiuwa nchi yetu. Hali hiyo inatuuwa kabisa," Alisema Trump. 

Trump pia alitoa madai ya kuwa "bora" katika mambo kadhaa, bila kutoa ushahidi. Wakati huo huo, Biden hakuridhisha sana katika mdahalo huo, akitoa majibu na sauti isiyo laini na wakati mwingine akionekana kuyapoteza Mawazo yake.

Wamarekani walifuatilia kwa karibu mdahalo huo wa kwanza wa telivisheni katika uchaguzi wa 2024 Picha: Scott Olson/Getty Images

Biden, Trump wakabiliana kuhusu Gaza na Ukraine

Mjadala wa sera ya kigeni uliangazia zaidi vita vya Gaza na Ukraine. Trump alidai kuwa uungaji mkono wa Washington kwa Ukraine unaumiza uchumi.

Soma pia: Biden na Trump kukabiliana katika mdahalo wa kwanza 2024

"Hii ni vita ambayo haikupaswa kuanza. Kama tungekuwa na kiongozi katika vita hivi... Ametoa dola bilioni 200 mpaka sasa au zaidi kwa Ukraine, ametoa dola bilioni 200. Hizo ni pesa nyingi sana. Sidhani kama kuna kitu kama hicho kilishawahi kutokea," Alisema Trump.

Lakini Biden alijibu kwamba msaada wa kijeshi kwa Ukraine ulitolewa kwa njia ya silaha zilizotengenezwa na Marekani, na kwamba mataifa mengine ya Magharibi kwa pamoja yametoa kiasi sawa cha misaada.

"Huyu ni mtu ambaye anataka kujiondoa katika NATO," Alisema Biden, na kuongeza kuwa "alipata mataifa mengine 50" kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Suala la umri lamulikwa

Hakukuwa na watazamaji katika ukumbi wa madahalo wa CNNPicha: Ben Hendren/Sipa USA/picture alliance

Biden na Trump ndio marais wenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuchaguliwa. Woze wanaulizwa maswali kuhusu uwezo wao wa kuwa rais kwa miaka mitano ijayo.

Akizungumza kwa sauti ya mkwaruzo aliyokuwa nayo katika muda wote wa mdahalo, Biden alisema aliingia Bunge la Congress kama mmoja wa maseneta wenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea.

Aliendelea kupigia debe orodha ya mafanikio yake kama rais na akabainisha kuwa Trump ni mdogo wake kwa "tofauti ya miaka mitatu tu.”

Katika majibu yake, Trump alidai kufaulu kwa urahisi vipimo vya utambuzi na kumwambia Biden naye akafanye vipimo hivyo.

Pia alijivunia uhodari wake wa kucheza gofu na kusema ana umbo zuri kama alivyokuwa miaka 25 iliyopita na labda sasa yeye ni "mwepesi kidogo."

Biden atilia mashaka maadili ya Trump

Biden alimshambulia Trump akitaka kuwakumbusha mamilioni ya watazamaji wa televisheni kuwa kama Trump atachaguliwa, atakuwa rais kwanza aliyehukumiwa kwa uhalifu kuingia White House.

Trump amesema azakubali matokeo ya uchaguzi kama anafikiri yatakuwa ya haki.

Afp, dpa, ap, reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW