Biden: Urusi haitashinda Ukraine
22 Februari 2023Matamshi hayo ameyatoa mjini Warsaw, Poland ikiwa ni saa kadhaa baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kusema Urusi itaendeleza mashambulizi yake ambayo yanakaribia kutimiza mwaka sasa.
Rais Biden akionekana wazi kujibu hotuba ya Rais Putin amesema mataifa ya Magharibi hayapangi njama ya kuishambulia Urusi.
Siku moja kabla ya kuyasema hayo, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80 alifanya ziara yake ya kwanza na ya kushtukiza mjini Kiev, tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza Februari 24, 2022 na ikiwa ni siku chache kabla ya kutimiza mwaka mmoja.
Awali katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Rais Putin aliyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kuongeza mzozo huo na kutangaza kuwa Urusi itasimamisha ushiriki wake katika mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia unaojulikana kama New START ambao iliusaini na Marekani.