Je, Big Tech zinatishia uhuru wa vyombo vya habari?
24 Juni 2026
Kwa zaidi ya miongo miwili, kampuni kubwa za teknolojia zimekuwa zikibadilisha kwa kasi namna habari zinavyozalishwa, kusambazwa na kutumiwa duniani. Kutoka kwenye injini za utafutaji, mitandao ya kijamii hadi mifumo ya akili mnemba (AI), kampuni hizo zimejijengea ushawishi mkubwa unaovuka sekta ya habari na kuingia moja kwa moja katika siasa, uchumi na maisha ya kila siku ya mabilioni ya watu.
Hali hiyo imekuwa mada kuu katika Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari la Deutsche Welle, Global Media Forum (GMF), linalofanyika mjini Bonn, Ujerumani. Washiriki zaidi ya 1,400 kutoka zaidi ya nchi 110 wamekutana kujadili namna vyombo vya habari vinaweza kulinda uhuru wake katika kipindi ambacho maendeleo ya teknolojia yanabadilisha kwa kasi mazingira ya habari.
Miongoni mwa mijadala iliyovutia umakini mkubwa ni ule uliopewa jina la "Between Innovation and Dependence: Journalism's Love-Hate Relationship with Big Tech,” yaani "Kati ya Ubunifu na Utegemezi: Uhusiano wa Upendo na Chuki kati ya Uandishi wa Habari na Kampuni kubwa za Teknolojia.”
Wadau walijadili maswali magumu: Je, kampuni kubwa za teknolojia ni washirika wa vyombo vya habari au ni washindani? Je, akili mnemba inatoa fursa mpya au inatishia uhai wa uandishi wa habari? Na ni nani anayepaswa kuwajibika kwa taarifa za uongo zinazozagaa mtandaoni?
Kwa wengi, majibu ya maswali hayo yatakuwa na athari kubwa katika mustakabali wa demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.
Je, Big Tech zina nguvu kiasi gani?
Sahana Udupa, mtaalamu wa anthropolojia ya vyombo vya habari, anaamini kuwa nguvu za kampuni hizo zimefikia kiwango kinachopaswa kutia wasiwasi.
Anasema kampuni hizo si tu zinamiliki majukwaa yanayotumiwa na mabilioni ya watu, bali pia zina uwezo wa kuathiri mijadala ya kisiasa na kijamii katika maeneo mbalimbali duniani.
"Makampuni haya yanaongoza mijadala ya kisiasa kwa dunia nzima. Hili linatia wasiwasi mkubwa. Tunahitaji kuzungumzia utofauti wa vyombo vya habari. Nafasi ya mitandao ya kijamii na akili mnemba inapaswa kuwa na mgawanyo mpana zaidi wa mamlaka kuliko ilivyo sasa. Kwa sasa tupo mikononi mwa kampuni chache kubwa.”
Kwa mtazamo wake, dunia imefikia hatua ambayo sehemu kubwa ya mawasiliano ya umma inategemea maamuzi ya kampuni chache za teknolojia. Hilo linaibua maswali kuhusu ushindani, uwajibikaji na uhuru wa kujieleza.
Wasiwasi huo uliungwa mkono na Courtney C. Radsch, Mkurugenzi wa Kituo cha Uandishi Habari na Uhuru cha nchini Marekani, ambaye alisema kuwa ushawishi wa kampuni hizo hauonekani tu katika miundombinu ya habari, bali pia katika namna wananchi wanavyoelekezwa kuona na kufikiria masuala mbalimbali.
Algorithimu zinachagua kwa niaba ya wananchi?
Kwa mujibu wa Radsch, madai kwamba majukwaa ya kidijitali yanawapa watu kile wanachotaka kuyaona si rahisi kuthibitishwa.
Anahoji iwapo watumiaji wa mitandao ya kijamii wanafanya maamuzi yao wenyewe au kama maamuzi hayo tayari yanaelekezwa na algorithimu zilizoundwa na kampuni hizo.
"Je, watu wana uchaguzi wa kile wanachokiona kwenye Instagram au kwenye mitandao yao ya kijamii? Au wanachagua kutokana na kile wanacholishwa? Ni vigumu kusema kwamba tunawapa watu kile wanachokitaka, wakati wengi hawakuwahi kukitaka hadi walipoanza kulazimishwa na algorithimu.”
Katika mjadala huo, Radsch alieleza pia kuwa ushawishi wa Big Tech umeongezeka kutoka kusambaza habari hadi kudhibiti mapato, mwonekano wa maudhui na hata namna akili mnemba inavyojifunza.
Kwa maoni yake, uandishi wa habari ni moja ya nyenzo muhimu zinazoiweka AI karibu na uhalisia. Bila taarifa za kuaminika zinazozalishwa na wanahabari, mifumo ya AI inaweza kuanza kujifunza kutokana na maudhui yaliyozalishwa na AI nyingine na hivyo kujitenga na ukweli.
Aliifananisha hali hiyo na kupiga picha ya nakala ya mchoro mara kwa mara, ambapo kila nakala mpya huondoka kidogo zaidi kutoka kwenye picha ya awali.
AI ni tishio au fursa?
Wakati baadhi ya washiriki wakionya kuhusu hatari za AI, wengine waliiona teknolojia hiyo kama fursa kubwa kwa vyombo vya habari.
Mwekezaji na mjasiriamali wa Silicon Valley, Cyriac Roeding, alisema vyombo vya habari vinapaswa kuacha kujiona kama wahanga wa mabadiliko ya teknolojia na badala yake vijifunze namna ya kunufaika nayo.
Alisisitiza umuhimu wa kuunda mifumo mipya ya biashara, kutumia teknolojia kwa ubunifu na kuwekeza katika maudhui yenye thamani.
Mtazamo huo uliungwa mkono kwa kiasi na Ramzi Rizk, kutoka kampuni ya Work in Progress Capital, ambaye alieleza jinsi AI inavyoweza kusaidia kupanua uwezo wa vyombo vya habari.
"Teknolojia hii inawawezesha watu ambao hawazungumzi lugha fulani kuunda maudhui katika lugha hiyo. Pia inasaidia majukwaa madogo kuwa ya lugha nyingi na kuendana na mahitaji ya kuandaa upya maudhui kwa hadhira tofauti.”
Kwa mujibu wa Rizk, uwezo huo unaweza kusaidia vyombo vya habari vidogo kufikia hadhira mpya bila kuhitaji uwekezaji mkubwa katika tafsiri au uzalishaji wa maudhui kwa lugha nyingi.
Hata hivyo, washiriki wengine walionya kuwa manufaa hayo hayatakuwa na maana ikiwa yatakuja kwa gharama ya uhuru wa habari au ubora wa taarifa.
Ulimwengu wa Tatu na changamoto za uendelevu
Mjadala huo pia uliangazia tofauti zilizopo kati ya nchi tajiri na zile zinazoendelea katika suala la ufadhili wa vyombo vya habari.
Marcela Duarte kutoka shirika la ukaguzi wa ukweli la Aos Fatos nchini Brazil alisema mifumo ya kulipia habari inayofanikiwa katika nchi za Magharibi haiwezi kuhamishwa moja kwa moja katika mazingira ya mataifa ya Kusini mwa Dunia.
Kwa mujibu wake, watu wengi katika nchi zinazoendelea wanakabiliwa na changamoto za msingi za maisha kiasi kwamba kulipia habari si kipaumbele kwao.
Alisema uandishi wa habari lazima uwafuate wananchi walipo, na kwa sasa wananchi wengi wanapatikana kwenye majukwaa ya Meta, Google na mitandao mingine ya kijamii.
Hilo linaonyesha utegemezi mkubwa uliopo kati ya vyombo vya habari na kampuni za teknolojia, hata wakati vyombo hivyo vikikosoa nguvu za kampuni hizo.
Taarifa za uongo na hatari kwa maisha
Mjadala ulipata sura tofauti wakati daktari na mwandishi wa habari za afya Eckart von Hirschhausen alipozungumzia athari za taarifa za uongo katika afya ya umma.
Alisema kuna watu wanaopoteza maisha kutokana na taarifa potofu zinazozagaa mtandaoni, hususan kuhusu chanjo na magonjwa ya kuambukiza.
Kwa mtazamo wake, suala la uwajibikaji wa majukwaa ya kidijitali si mjadala wa biashara pekee bali ni suala la maisha na kifo.
Hirschhausen alitaka kampuni za teknolojia kuwajibishwa zaidi kwa maudhui yanayosambazwa kupitia mifumo yao na kuhimiza kujengwa kwa mazingira ya kidijitali yanayoongozwa na maadili ya umma badala ya maslahi ya kibiashara pekee.
Wakati wa kongamano la Global Media Forum mjini Bonn, jambo moja lilionekana kuwa wazi: akili mnemba na Big Tech zimekuwa sehemu muhimu ya mazingira ya habari duniani. Swali ni jinsi ya kuhakikisha kuwa maendeleo hayo yanaimarisha badala ya kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia.