1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bill Gates atoa msaada kwa ajili ya utafiti wa AIDS.

Sekione Kitojo20 Julai 2006

Wakfu wa Bill Gates na mkewe Melinda Gates umetangaza kiasi cha dolla milioni 287 siku ya Jumatano ili kuunda mfumo wa kimataifa wa maabara 16 zitakazojaribu njia mpya za kutengeneza chanjo dhidi ya ukimwi.

Wakfu huo unasema kuwa unataka mpango huo kubadilisha juhudi za hivi sasa ambazo zimeshindwa za chanjo ya ukimwi kwa kuyapa maabara binafsi ambayo yatakuja na mawazo mapya na kuyasaidia kuendeleza mawazo hayo, lakini pia kuhakikisha kuwa wanashirikiana na watafiti wengine, ambao chini ya hali ya kawaida wangeonekana kuwa ni wenye kupigania maslahi ya aina moja.

Huu ni uwekezaji mkubwa kabisa kuwahi kufanywa na wakfu huo katika utengenezaji wa chanjo ya ukimwi. Kwa hakika , ni mpango wetu mkubwa kabisa wa misaada kwa ajili ya ukimwi na HIV, Dr. Nicholas Hellmann, kaimu mkurugenzi wa wakfu wa Bill Gates unaohusika na masuala ya magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu, na mpango wa afya katika uzazi, amewaambia waandishi wa habari.

Ukimwi uliweza kufahamika katika mwaka 1981 na virusi vinavyofanya mwili kukosa kinga yake ya asili ambavyo vinasababisha AIDS viligunduliwa mara baadaye, lakini imeonyesha kuwa ni vigumu mno kuweza kupata njia ya kutengeneza chanjo inayoweza kuleta nafuu.

Virusi hivyo hushambulia celi zinazofanyakazi kuulinda mwili ambazo kwa kawaida huzinduliwa na chanjo, na hubadilika haraka na kuzuwia nguvu zinazotokana na mwili wa binadamu za kupambana kwa haraka na magonjwa. Zaidi ya chanjo 30 zinajaribiwa kwa watu hivi sasa, lakini hakuna mwanasayansi anayetarajia kuwa moja kati ya hizo zinaweza kuzuwia maambukizo ya HIV kwa kiwango kikubwa cha watu.

Matarajio makubwa kutokana na mwelekeo wa sasa ni pengine kuchelewesha maambukizi, ama kuyafanya maambukizi yasiyokuwa na athari kubwa zaidi kwa baadhi ya watu.

Misaada hiyo 16 itakwenda kwa zaidi ya watafiti 165 katika nchi 19, ambazo baadhi yao ni majina makubwa katika utafiti wa AIDS na baadhi wale wasio na majina makubwa katika kazi hiyo,

Wakati maelfu ya wajumbe kutoka duniani kote wakijikusanya mjini Toronto mwezi ujao kwa ajili ya mkutano wa 16 wa kimataifa wa AIDS, makundi ya kutetea haki za binadamu yameutaka mkutano huo kuangalia masuala ya wahanga wa ugonjwa huo wanavyouwawa.

Mauaji ya Vivian Kavuma mwezi Juni nchini Uganda yaliyofanywa na mpenzi wake baada ya kugundua kuwa ameambukizwa HIV.

Kuchomwa visu kikatili kwa Isaiah Gakuyo mwenye umri wa miaka 15 Aprili mwaka jana nchini Kenya na mjomba wake kwa sababu eti yatima huyo alikuwa nae na ugonjwa wa HIV. Orodha haiishii hapo ni ndefu.

Tunayo maarifa ya kupambana na AIDS hivi sasa , tunajiu kile ambacho kinaweza kufaa, na hiyo ni kukubali kuwa janga hilo linasababishwa na kuendewa kinyume haki za binadamu, suala ambalo linazidisha janga hilo, Joseph Amon , mkurugenzi wa mpango wa HIV/AIDS katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ameliambia shirika la habari la IPS.

Tangu pale ugonjwa huo ulipogundulika kwa mara ya kwanza mapema katika miaka ya 1980 HIV/AIDS imesababisha vifo vya watu milioni 22 na kuwaambukiza wengine milioni 60. Mwaka ulipita ,watu milioni tano waliambukizwa na milioni tatu wamekufa kutokana na ukimwi.

Kati ya mwaka 2003 na 2005 , idadi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi katika Asia ya mashariki ilipanda kwa zaidi ya asilimia 25 na idadi ya watu wanaoishi na virusi hivyo katika Ulaya ya kati na Asia ya kati imepanda kwa zaidi ya theluthi moja.

Lakini kwa mujibu wa Human Rights Watch na wengine , katika miaka 25 tangu kugunduliwa kwa AIDS, nchi chache zimefanikiwa kudhibiti janga hilo. Wale ambao wamefanikiwa wametoa taarifa sahihi juu ya maambukizi ya HIV kwa wananchi wake, wameangalia udhaifu wa wanawake na wasichana katika masuala ya utumiaji nguvu na uendeaji kinyume, wamehakikisha mipira ya ngono inapatikana , sindano salama na dawa, na kueneza dawa za kurefusha maisha kwa wale ambao tayari wameambukizwa.

Wataalamu wanasisitiza kuwa udhaifu katika HIV/AIDS unahusishwa kwa karibu na utaratibu wa kimaisha wa jamii husika kuwatenga watu walioambukizwa virusi hivyo. Hawa ni pamoja na wasichana wadogo, watumiaji wa mihadarati, watu wanaoshughulika na kutoa huduma ya ngono, wanaume ambao wanafanya mapenzi na wanaume wenzao, wahamiaji na wafungwa pamoja na uendeaji kinyume mwingine haki za binadamu.