1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BioNTech inapanga kufungua kiwanda chake Afrika

16 Februari 2022

Kampuni ya kutengena chanjo ya Ujerumani BioNTech ambayo kwa ushirikiano na Pfizer ilitengeneza chanjo ya kwanza iliyoidhinishwa dhidi ya COVID19 imetangaza mpango wa kuanzisha vituo vya utengenezaji chanjo barani Afrika

Symbolbild Coronaspritze und einer Hand mit einem Gummihandschuh
Picha: Fleig/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Muundo wa vituo hivyo uliowasilishwa katika sherehe huko Marburg nchini Ujerumani, unajumuisha vyombo vya usafirishaji vilivyowekwa vifaa muhimu vya kutengenezea chanjo ya mRNA kutoka mwanzo hadi mwisho, ispokuwa hatua ya mwisho ya kujaza dozi za chanjo kwenye chupa.

BioNTech imekuwa ikikosolewa na baadhi ya vikundi vya wanaharakati kwa kukataa kusitisha vibali vyake vya chanjo na kuruhusu kampuni nyengine kutengeneza chanjo hiyo, kama sehemu ya jitihada ya kuzifanya zipatikane kwa wingi zaidi hasa katika nchi maskini.

Mkurugenzi Mtendaji wa BioNTech Ugur Sahin ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, lengo leo ni kuwezesha utengenzaji wa chanjo za mRNA duniani kote. Lakini Sierk Poetting mkuu wa kitengo cha masuala ya kiufundi wa kampuni ya BioNTech amesema hatua ya kwanza itakuwa barani Afrika.

''Kimsingi, teknolojia hii inaweza kutumiwa popote. Bara la Afrika litakuwa la kwanza kunufaika, kwa sababu tumejifunza somo kubwa wakati huu wa janga la corona, juu ya malumbano na matatizo katika zoezi la usambazaji wa chanjo. Matatizo hayo unaweza kuyaepusha tu, ikiwa utatengeneza chanjo katika nchi husika,'' alisema Sierk Poetting

Hata hivyo kampuni hiyo inadai pia kuwa mchakato wa kutengeneza chanjo za mRNA ni mgumu mno na inapendelea kufanya kazi na washirika wa ndani ili kuhakikisha ubora ulio thabiti duniani kote.

WHO yausifia mpango wa BioNTech

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Fabrice Coffrini/KEYSTONE/picture alliance

Kituo cha kwanza na kilicho kamili cha utengenezaji chanjo kitasafirishwa hadi nchini Senegal, Rwanda au Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka huu. BioNTech imesema inalenga kuanza utengenzaji wa hadi dozi milioni 50 za chanjo kwa mwaka ndani ya miezi 12 ijayo huku ikisubiri idhini kutoka mamlaka za ndani. BioNTech imesema mfumo huo, ambao una makontena 12, unaweza kurekebishwa kwa urahisi katika siku zijazo na hivyo kusaidia kutengeneza chanjo dhidi ya magonjwa mengine yaliyosambaa barani Afrika kama vile malaria au kifua kikuu.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameusifia mpango wa BioNTech wa kuongeza uzalishaji wa chanjo barani Afrika, akisema bila shaka utasaidia juhudi za kukuza matumizi ya teknolojia ya mRNA nchini Afrika Kusini na kwengineko.

Hapo awali BioNTech imesema itashughulikia kwanza upatikanaji wa vifaa na baadaye ihamishe ujuzi wao kwa washirika wa ndani ili kuwezesha operesheni hiyo kujitegemea kikamilifu. Chanjo zitakazotengenezwa huko zitatumiwa katika nchi husika na hata mataifa mengine ya Umoja wa Afrika kwa bei nzuri na isiyolenga faida.

Licha ya juhudi za kutoa mamilioni ya dozi ya chanjo ya COVID-19 kwa bara la Afrika kupitia mfumo wa kimataifa wa wafadhili, ni takriban asilimia 11 tu ya watu katika bara hilo ambao wamepokea dozi moja ya chanjo, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa karibu asilimia 50.

Michel Sidibe, Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika kwa Muungano wa Shirika la Madawa la Afrika amesema, kwa kuzingatia kuibuka na kuenea kwa aina mpya ya virusi, hatutoondokana na janga hili hadi limalizike kila mahali, huku akiongeza kuwa ana matumaini mpango huo utazidisha uzalishaji wa chanjo ya mRNA barani Afrika.

Chanzo: afp,reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW