Blair, Lebanon yaandamana na kumsusia.
11 Septemba 2006Blair alikuwa anawasili mjini Beirut kutoka nchini israel, katika ziara yake ya mashariki ya kati tangu kumalizika kwa vita vya wiki nne baina ya Hezbollah na Israel.
Muda mfupi tu baada ya ndege ya Balir, kutua katika uwanja wa ndege wa Beirut, maelfu ya waandamanaji walimiminika mabarabarani kupinga ziara hiyo na kumshtumu Blair.
Iliwabidi polisi kupiga doria eneo la mkutano kati ya Balir na mwenyeji wake waziri mkuu wa Lebanon Fuad Siniora.
Lakini haikuwa hoja, baadhi ya waandamanaji waliingia mkutano na kumpigia makelele Blair, huku wakiwa wamebeba mabango wakimsuta Blair, baada ya Uingereza kukataa kuishurutisha Israel kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia wa Lebanon.
Kwa upande wake Blair alisisitiza kuwa, la muhimu ilikuwa sio kusitisha uhasama tu, bali kutafuta suluhu ya kudumu, na ndio maana walishinikiza kupitishwa kwa azimio la 1701 katika Umoja wa Mataifa.
Na hapa ndipo akaahidi kuwa Uingereza italisaidia jeshi la Lebanon, ambalo limepelekwa kusini mwa nchi hiyo kuchukua nafasi zilizokuwa zimeshikiliwa na wanamgambo wa Hezbollah.
" Ni muhimu kwa jeshi la Lebanon kuwa na nguvu ya udhibiti wa nchi nzima ya Lebaon, sisi kama Uingereza tutatoa msaada wowote, wa kifundi na vifaa kulisaidia jeshi la Lebanon." alisema Balir
Blair alikubali kuwa sera zake ziliwakera watu wengi, lakini akasisitiza kuwa daima amekuwa akizipa kipau mbele harakati za kupatikana kwa amani ya kudumu mashariki ya kati.
Lakini haikuwa tu maandamano, baadhi ya maafisa wakuu nchini Lebanon walikataa kukutana na Blair. Kwa mfano spika wa bunge Nabih Berri ambaye alipangiwa kukutana na Blair alisemekana kuwa amesafiri nje ya nchi, ilhali baadhi ya mawaziri wakiwemo wawili wanaounga mkono Hezbollah walisusia kukutana na Blair.
Msimamo wa Blair mashariki ya kati umekosolewa kufuatia yeye kuunga mkono sera za Marekani na Israel. Akiwa nchini Israel siku ya Jumamosi, kundi la Hamas lilikatalia mbali pendekezo la Blair kuwa waungane na rais Mahmoud Abbas kuunda serikali ya muungano ili waomndolewe vikwazo walivyowekewa na jumuiya ya kimatifa.
Wakati huo huo, Ujerumani sasa imepata mualiko rasmi wa kuwapeleka wanamaji wake nchini Lebanon, kama mchango wake katika jeshi la Umoja wa Mataifa. Mualiko huu sasa utachambuliwa na bunge las Ujerumani kabla ya kuidhinishwa na waziri mkuu Bi Angela Merkel.