Blair na Chirac bado wavutana kuhusu bajeti ya umoja wa Ulaya.
15 Juni 2005Matangazo
Brussels:
Siku moja kabla ya mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, mzozo kuhusu bajeti ya umoja huo kuanzia 2007 hadi 2013 bado unaendelea bila ya suluhisho. Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair na Rais wa Ufaransa Jacques Chirac walishindwa hapo jana kuondoa tafauti zao wakati wa mazungumzo yao mjini Paris. Kufuatia mazungumzo hayo Bw Blair alisema pande hizo mbili bado ziko mbali mno. Rais Chirac amekua akidai nafuu iliopewa Uingereza katika mchango wake wa bajeti ifutwe, huku Bw Blair naye akitaka paweko na mabadiliko katika sera ya pamoja ya kilimo ikiwa ni pamoja na mtindo wa Ufaransa wa kufidia wakulima wake. Lakini takwa hilo la Blair linapigwa na Ufaransa na Ujerumani.