Blatter atofautiana na wafadhili wa FIFA
31 Oktoba 2015Kiongozi huyo aliyesimamishwa kufanya shughuli za soka kwa miezi mitatu amesema hatua hiyo ilikuwa na hamasa za kisiasa na ilichukuliwa kwa kushinikizwa na Marekani.
Blatter amezuiwa kushiriki katika shirikisho la FIFA ikiwa ni sehemu ya kutofautiana na uchunguzi wa wizara ya sheria ya Marekani kuhusiana na rushwa, kusafisha fedha na udangayifu mbali mbali katika shirikisho hilo la kandanda.
Blatter mwenye umri wa miaka 79 awali alikuwa abakie madarakani hadi mwaka ujao, licha ya maafisa kadhaa wa FIFA wa ngazi ya juu kukamatwa, hadi pale wafadhili wakubwa walipotoa miito ya pamoja kuondolewa madarakani kwa kiongozi huyo. Blatter alisitishwa kufanyakazi zake katika FIFA siku chache baadaye.
"Ni makampuni ya Marekani, " Blatter ameliambia gazeti la Financial Times katika mahojiano akilenga lawama hizo kwa makampuni ya Coca cola, McDonald, Visa na Budweiser.
Blatter na kiongozi wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA Michel Platini wote wanatumikia adhabu ya siku 90 ya kusimamishwa kufanya shughuli za kandanda adhabu iliyotolewa na kamati ya maadili ya FIFA , ambayo inaangalia kuhusu dola milioni 2.03 zilizotolewa na Blatter kwenda katika akaunti ya Platini mwaka 2011, kesi ambayo pia ni sehemu ya uchunguzi tofauti wa maafisa wa Uswisi.
Blatter pia amerudia madai kwamba kuingilia kati kwa serikali ya rais wa wakati huo Nicolas Sarkozy wa Ufaransa kumesababisha Qatar kupewa jukumu la kuandaa mashindano ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2022 badala ya Marekani. Akizungumza na gazeti hilo la Uingereza, Blatter amerudia madai aliyoyatoa siku ya Jumatano kwa shirika la habari la Urusi TASS kwamba kamati tendaji ya FIFA ilikubaliana kimsingi kuipa Urusi mashindano ya mwaka 2018 na yale ya mwaka 2022 kwa Marekani.
Wakati huo huo mkuu wa kamati ya matayarisho ya kombe la dunia mwaka 2018 amekana kwamba kupewa fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kulipangwa.
Na pia Urusi haitapunguza tena bajeti ya mashindano hayo, amesema waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko wakati akizungumza na shirika la habari la Urusi TASS.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae /rtre / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu