Blinken aelekea Asia na Ulaya katika ziara yake ya mwisho
4 Januari 2025Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, anaelekea barani Asia na Ulaya mwishoni mwa juma hili katika ziara inayotarajiwa kuwa ya mwisho nje ya nchi.
Blinken atazuru Korea Kusini, Japan na Ufaransa kuanzia kesho Jumapili. Atarejea Washington mapema Alhamisi kuhudhuria mazishi ya Rais wa zamani Jimmy Carter.
Nchini Korea Kusini na Japan, Blinken anakusudia kuangazia upanuzi wa ushirikiano wa Marekani na mataifa yote mawili kama sehemu ya mkakati wa utawala wa Biden wa Indo-Pacific.
Mkakati huo kimsingi ulikusudiwa kufifisha matarajio ya China katika eneo hilo lakini pia kuzuia tishio la nyuklia kutoka kwa Korea Kaskazini.
Blinken anazuru Korea Kusini, iliyokumbwa na mtikisiko wa kisiasa kufuatia hatua ya rais Yoon Suk-yeol kutangaza sheria ya kijeshi na baadaye kushtakiwa.