1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aiambia Israel iepuke 'madhara zaidi kwa raia' Gaza

9 Januari 2024

Zaidi ya miezi mitatu tangu kuanza kwa vita vikali zaidi Gaza, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony Blinken aliitaka Israel siku ya Jumanne "kuepuka madhara zaidi ya kiraia" katika eneo la Palestina lililozingirwa.

Israel | Ziara ya waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Tel Aviv
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akisaliamiana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv.Picha: Antony Blinken Office/ZUMA Wire/IMAGO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alikutana na viongozi wa Israel siku ya Jumanne, katika juhudi zake za kupunguza makali ya mzozo wa Gaza, na kuwaambia kuwa bado kuna nafasi ya taifa hilo kukubaliwa na majirani zake wa Kiarabu, endapo watatengeneza njia ya kuunda taifa la Palestina.

Akiwa katika ziara yake ya nne ya Mashariki ya Kati tangu mwezi Oktoba, katika juhudi za kudhibiti mzozo, ambazo kwa sehemu kumbwa zimeambulia patupu, waziri Blinken alisema amewashirikisha viongozi wa Israel, kile alichosikia katika siku mbili za mazungumzo na Jordan, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia.

Blinken alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benajmin Netanyahu, na kuzungumza na wajumbe wa baraza la vita lililoundwa baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas, ambayo Israel inasema yaliuwa watu 1,200.

Soma pia: Blinken aona fursa kwa Israel kushirikishwa kikanda

Mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya Wapalestina 23,000, kuharibu sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, na kuwalazimisha idadi kubwa zaidi ya wakaazi wa Gaza kuyahama makazi yao, hali iliyozusha mzozo mkubwa na unaozidi kuwa mbaya wa kibinadamu.

Waziri Blinken ameiambia Israel iepushe madhara kwa raia katika vita vyake Gaza.Picha: ABIR SULTAN/AFP

Tayari Blinken amesema ataishinikiza Israel kuhusu ulaazima wa kuwalinda raia wa Gaza na kuruhusu misaa ya kiutu kuwafikia. Mkuu wake, Rais Joe Biden, alisema Jumatatu usiku mjini Washington, kwamba alikuwa akiishinikiza kimya kimya Israel kuanza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake Gaza.

Mikutano ya Blinken katika kanda ya Mashariki ya Kati imejikita zaidi kwenye kutafuta mkakati wa muda mrefu wa kutatu mzozo wa miongo mingi wa Israel na Palestina, kama sehemu ya njia ya kuelekea kumaliza vita vya Gaza.

Msisitizo juu ya kuundwa kwa taifa la Palestina

Baada ya mikutano yake na washirika wa Kiarabu, alisema walitaka kutaka ushirikiano na Israel, ambao pia ndiyo lengo la muda mrefu la Israel, lakini iwapo tu hilo linahusisha njia ya kweli ya kuundwa kwa taifa la Palestina.

"Mustakabali wa kanda hii unatakiwa kuwa wa ushirikiano, sio mgawanyiko na mzozo. Na kwa hilo kutokea, tunahitaji kuona uanzishwaji wa taifa huru la Palestina," alisema Blinken alipozungumza na rais wa israel Isaac Herzog.

Soma pia: Afrika Kusini yaishtaki Israel ICJ kwa 'mauaji ya kimbari' Gaza

"Sasa, hakuna niliyezungumza anaefikiri hii itakuwa rahisi. Sisi sote tunatambua vizingiti na hakuna mtu anayefikiri kwamba chochote kitatokea mara moja. Lakini tulikubaliana kufanya kazi pamoja."

Akizungumza mjini Cairo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, amesisitiza pia haja ya kupunguza makali ya vita, huku akirejelea msimamo wa Berlin wa kuiunga mkono Israel bila kuyumba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumanim Annaelna Baerbock akizuru kivuko cha Rafah, kati ya Misri na Gaza, wakati wa ziara yake nchini Misri, Januari 09, 2024.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mwezake wa Misri, Sameh Shoukry, ameelezea wasiwasi juu ya kuwahamisha Wapalestina, na kusema watu milioni mbili hawawezi kubaki wamenaswa katika sehemu moja kusini kwa njia hiyo.

Baada ya wiki kadhaa za shinikizo la Marekani kulegeza mashambulizi, Israel inasema vikosi vyake vinahama kutoka vita kamili hadi kwenye kampeni ya kulenga kaskazini mwa Gaza, wakati likiendeleza mapambano makali katika maeneo ya kusini. 

Soma piaIsrael, Hizbullah washambuliana tena

Hii leo jeshi hilo limesema limeua karibu wapiganaji 40 wa Kipalestina, na kuvamia eneo la kijeshi na mahandaki tangu Jumatatu katika mji wa Khan Younis, ulioko kuisni mwa Gaza.

Jeshi hilo limesema pia Jumanne kwamba wanajeshi wake wasiopungua tisa wameuawa Gaza, wengi wao kutoka kitengo cha uhandisi kinachoendelea shughuli zake katika mahandaki ya Gaza, katika mmoja ya siku zenye maafa makubwa zaidi ya operesheni yake ya ardhini.

Vifo hivyo vinafikisha jumla ya wanajeshi 187 kwa mujibu wa takwimu zake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW