1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken akutana na rais Abdel Fattah el-Sissi

26 Mei 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi kabla ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sameh Shukry na mkuu ujasusi  Abbas Kamel.

Israel Jerusalem | US Außenminister Blinken
Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

 

Blinken aliwasili nchini Misri siku ya Jumatano siku moja baada ya kufanya mazungumzo ya kina na viongozi wa Israeli na Palestina.

Blinken alikutana na rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi na viongozi wengine wakuu serikalini. Blinken ameahidi kushinikiza usaidizi wa kimataifa kujenga upya eneo la ukanda wa Gaza lililoharibika kutokana na mashambulizi ya Israeli  huku akiahidi kuhakikisha kuwa hakuna msaada unaotolewa kwa ajili ya eneo hilo unalifikia kundi la Hamas. Badala yake, amesema kuwa wanajaribu kuimarisha mamlaka ya Palsetina inayotambulika kimataifa.

Blinken ameitaja Misri na Jordan kama wadau muhimu katika kujaribu kuleta utulivu katika kanda hiyo. Mataifa yote mawili ni washirika muhimu wa Marekani yaliyo na mikataba ya amani na Israeli na mara kwa mara hutumika kama wapatanishi kati ya Israeli na Palestina.

Rais wa Misri- Abdel-Fattah el-SissiPicha: picture-alliance/AP Photo/MENA

Hatua iliyochukuliwa na Misri

Misri imetuma ujumbe wake nchini Israeli na katika ukanda wa Gaza kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na pia imekuwa ikisimamia misaada ya kimataifa na msaada wa kujenga upya kwa eneo hilo la Palestina ambalo limekaliwa na Israeli kwa takriban miaka 15.

Blinken amesema leo kuwa Marekani iko katika harakati ya kutoa msaada zaidi wa dola milioni 360 za msaada kwa watu wa Palestina. Hii inajumuisha dola milioni 250 katika maendeleo ya kiuchumi, ulinzi, na msaada wa kiutu uliotangazwa katika miezi ya Machi na Aprili.

Mbali na hayo, serikali ya nchi hiyo inanuia kutoa dola milioni 75 zaidi kuwasaidia Wapalestina pamoja na dola milioni 5.5 kwa usaidizi wa dharura wa kushughulikia majanga katika ukanda wa Gaza pamoja na dola milioni 33 kwa ombi la dharura la

msaada wa kiutu lililotolewa na shirika la wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa. Wiki iliyopita, Sissi aliahidi dola milioni 500 kusaidia katika juhudi za kujenga upya ukanda wa Gaza.