1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Blinken akutana na Rais Erdogan katika ziara yake Uturuki

Sylvia Mwehozi
20 Februari 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesisitiza dhamira ya Washington ya kuipatia Uturuki ndege za kijeshi aina ya F-16 wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake nchini humo.

Türkei | Besuch US Außenminister Antony Blinken in Ankara
Picha: Burhan Ozbilici/AFP/Getty Images

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Blinken kuitembelea Uturuki ambayo ilikuwa imepangwa kabla ya kutokea tetemeko la ardhi mnamo Februari 8 na kusababisha vifo vya watu karibu 45,000.

Uhusiano baina ya Uturuki na Marekani umeingia dosari katika miaka ya hivi karibuni, lakini Washington inaichukulia Ankara kuwa na umuhimu katika juhudi za upatanishi baina ya Urusi na Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi karibu mwaka mmoja uliopita.

Mapema leo Jumatatu, Blinken amefanya mazungumzo na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambapo waligusia vita vya Ukraine na "umuhimu wa kufanya kazi kwa ukaribu" katika masuala yanojumuisha ulinzi, nishati na usalama wa pamoja.WASHINGTON : Marekani kuiuzia Pakistan ndege za F-16

Antony Blinken naMevlut Cavusoglu walipotembelea eneo lililoathiriwa na tetemeko la ardhiPicha: Clodagh Kilcoyne/AP/picture alliance

Mojawapo ya masuala makuu katika ziara hiyo ilikuwa ni shauku ya Uturuki kununua toleo la karibuni la ndege za kivita chapa F-16 kutoka Washington. Bunge la Marekani linazuia uuzwaji wa ndege hizo kutokana na wasiwasi wa rekodi ya Uturuki ya ukandamizaji wa haki za binadamu na vitisho kwa Ugiriki.

"Kuhusu ndege za F-16, utawala wa Biden unaunga mkono kwa dhati uboreshwaji wa ndege za F-16 zilizopo na kutoa mpya kwa Uturuki kwa sababu kama mshirika wa NATO, ni kwa maslahi yetu ya kitaifa na usalama wa muungano ambao Uturuki anaendelea kufanya kazi katika viwango vya juu vya NATO na kuhakikisha kuwa tuna uwezo kamili usioingiliwa," alisema Blinken.

Suala jingine lililojadiliwa wakati wa ziara ya Blinken ni Uturuki kukataa kuidhinisha ombi la Sweden na Finland kujiunga na Jumuiya ya Kujihami NATO.

Nchi hizo mbili ziliachana na sera yake ya miongo kadha ya kutofungamana kijeshi na kuomba kujiunga na jumuiya hiyo inayoongozwa na Marekani kufuatia uvamizi wa Moscow dhidi ya Ukraine.

Ankara imekuwa ikiikosoa  Sweden kwa kushindwa kuwarejesha washukiwa kadhaa wanaohusishwa na wanamgambo wa Kikurdi pamoja na mapinduzi ya yaliyoshindwa ya mwaka 2016.

Picha kutoka angani inayoonyesha majengo yaliyoporomoka UturukiPicha: Clodagh Kilcoyne/REUTERS

Blinken amesema kuwa Marekani "inaunga mkono kwa nguvu zote" mataifa hayo mawili kupewa uanachama wa NATO "haraka iwezekanavyo," akisema nchi hizo mbili zimechukua hatua za kutosha kushughulikia wasiwasi wa Ankara. Lakini Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki Mevlut Cavosoglu anasema hakupaswi kuwa na masharti juu ya kuidhinishwa kwa ununuzi wa ndege za F-16 wala kulihusisha suala hilo na maombi ya Sweden na Finland.Finland yatumai kukubaliana na Uturuki kuhusu NATO

Uturuki imeashiria kuwa iko tayari kuikubalia Finland kujiunga na NATO, lakini kwa mujibu wa Cavusoglu ni kwamba wanamgambo wa Kikurdi bado wanaendelea na "shughuli za kila aina ikiwa ni pamoja na kuajiri na propaganda za kigaidi" nchini Sweden.

Blinken ambaye amezuru Uturuki kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe miaka miwili iliyopita, hapo jana aliwatembelea wanajeshi wa Marekani na Uturuki sambamba na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu karibu na Adana waliokuwa katika shughuli ya utoaji usaidizi muhimu kwa maeneo yaliyoathirika na tetemeko. Blinken ameahidi msaada wa dola milioni 1000 kusaidia Uturuki na Syria ikiwa ni nyongeza ya Dola milioni 85 zilizotangazwa na Rais Joe Biden kwa nchi zote mbili.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW