Blinken akutana na Rais wa Misri kujadili mizozo ya kikanda
30 Januari 2023Akiwa mjini Cairo, Antony Blinken amekutana na Rais Abdel Fattah al-Sisi na Waziri wa Mambo ya Nje Sameh Shoukry.
Mazungumzo yao yanalenga kujadili masuala ya kikanda ikiwa ni pamoja na kutuliza mzozo baina ya Israel na wapalestina, kufufua upya mazungumzo ya kisiasa nchini Sudan na kushughulikia msuguano kati ya makundi hasimu nchini Libya.
Baadae Blinken anatarajiwa kwenda Jerusalem, ambako atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huku kukiwa na wasiwasi ndani na nje ya nchi kuhusu sera za serikali mpya ya mrengo wa kulia ya Netanyahu.
Katika ziara yake hiyo ya siku tatu Mashariki ya Kati, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, pia atasafiri hadi Ramallah kukutana na Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas.
Soma pia:Wanajeshi Israel wamuua kwa risasi mwanaume wa Kipalestina
Ziara hiyo ya Blinken imekuja wakati ghasia zimeongezeka baina ya Israel na Wapalestina. Wizara ya afya ya Palestina imesema leo kwamba wanajeshi wa Israel wamemuua Mpalestina katika Ukingo wa Magharibiunaokaliwa kwa mabavu na Israel.
Taarifa ya wizara hiyo imesema Mpalestina, Nassim Abu Fouda, mwenye umri wa miaka 26, aliuwawa kwa kupigwa risasi kwenye mji wa Hebron.
Eneo hilo mara nyingi hutazamwa kama kitovu cha machafuko kati ya jeshi la Israel na Wapalestina. Mauaji hayo ni ya hivi karibuni katika ongezeko la umwagaji damu katika eneo hilo.
Hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa jeshi la Israel kufuatia kisa hicho.
Blinken anahimiza 'utulivu' katika mzozo wa Mashariki ya Kati
Ghasia kati ya Israel na Palestina zimeongezeka katika siku za hivi karibuni, na wiki iliopita jeshi la Israel lilivamia ngome ya wanamgambo katika mji wa Jenini ulioko Ukingo wa Magharibi.
Katika uvamizi huo watu kumi waliuwawa, wengi wao wakiwa wanamgambo, na Wapalestina walishambulia kwa risasi makazi ya Wayahudi mjini Jerusalem mashariki ambako waliwaua Waisraeli saba.
Soma pia:Israel yashambulia Gaza baada ya wanamgambo kurusha roketi
Ziara ya Blinken, ambayo ilipangwa kabla ya kuzuka kwa machafuko haya mapya, ilikuwa
inatarajiwa kujaa mvutano juu ya tofauti kati ya utawala wa Bidenna Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu serikali mpya, ambayo inaundwa na wafuasi wa sera ya ujenzi wa makaazi.
Blinken sasa anahitaji kukabiliana na changamoto ya ziada wakati wa safari yake, kujaribu kurejesha utulivu hata kama vurugu zinaendelea. Baada ya shambulio la Jenin, Wapalestina walisema watathmini
uratibu wa usalama na Israeli. Na baada ya mashambulizi dhidi ya Waisraeli kuongezeka, Israel pia ilisema itaimarisha makazi ya Wayahudi katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi, kati ya hatua zingine.