1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aonya kuhusu haki za binaadamu, India

28 Julai 2021

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken Jumatano hii amefanya mazungumzo na viongozi waandamizi nchini India katika mikutano inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano.

USA Anthony Blinken in Indien Neu Delhi
Picha: JONATHAN ERNST/REUTERS

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken hii leo amefanya mazungumzo na viongozi waandamizi nchini India, katika mikutano inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano baina ya washirika hao wawili ambao kwa pamoja wana mtizamo unaofanana dhidi mpinzani wao na anayezidi kujiimarisha, China 

Anthony Blinken pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa India Subrahmanyam Jaishankar walitarajiwa kujikita zaidi katika majadiliano kuhusiana na kuimarisha mahusiano baina yao, na kitisho cha China, lakini pia rekodi ya hivi karibuni ya hali ya kibinaadamu nchini India pamoja na masuala yanayohusiana na janga la COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi.

Ajenda kuhusiana na mkutano wa kilele wa muungano wa masuala ya usalama wa Quad, unaoyakutanisha mataifa ya Marekani, India, Australia na Japan ambao huenda ukafanyika nchini Marekani baadaye mwaka huu pia ilitarajiwa kujadiliwa. Mataifa chini ya muungano huo pia yanasaidiana katika kukabiliana na kujiimarisha kwa China kiuchumi na kijeshi na Marekani kwa muda mrefu unamuangalia India kama mshirika mkuu katika jitihada za kuzuia kujiimarisha wa China kwenye ukanda wa India na Pasifiki.

Blinken aonya kuhusu rekodi ya haki za binaadamu nchini India.

Kabla ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni Jaishankar, Blinken anayezuru kwa mara ya kwanza New Delhi alifanya mazungumzo ya faragha na mshauri wa masuala ya usalama wa India Ajit Doval, ingawa haijulikani ni masuala gani hasa waliyojadiliana.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken akizungumza na wawakilishi wa mashirika ya kiraia nchini India.Picha: JONATHAN ERNST/REUTERS

Awali, Blinken alifanya mazungumzo na viongozi wa mashirika ya kiraia na kuonya kuhusiana na kuporomoka kwa demokrasia nchini India, kufuatia madai ya makundi ya haki za binaadamu ya kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya wakosoaji na kuminywa kwa demokrasia.

Blinken Amesema, "Tumeunganishwa na maadili ya pamoja na naamini, matakwa ya pamoja ambayo ni ya kawaida kwa watu wetu. Watu wa India na Amerika wanaamini katika utu na usawa wa fursa, sheria, misingi ya uhuru na uhuru wa imani ya dini. Tunaamini kwamba watu wote wanastahili kuwa na sauti kwa serikali yao na kutendewa kwa heshima, bila kujali ni akina nani. Hii ndio misingi ya demokrasia kama yetu."

Akutana na mwakilishi wa Dalai Lama.

Chini ya utawala wa waziri mkuu Narendra Modi, India imekuwa ikitumia kwa kiasi kikubwa sheria dhidi ya ugaidi kuwakatama wapiga kampeni, waandishi wa habari, wanafunzi na wengine, hii ikiwa ni kulingana na wakosoaji, ingawa serikali inakana madai hayo, ikisema watu wote wana haki sawa.

Aidha Blinken amekutana na mwakilishi wa kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama hatua ambayo huenda ikaibua ghadhabu nchini China. Blinken amekutana kwa muda mfupi na mwakilishi huyo Ngodup Dongchung. Ikumbukwe kwamba mnamo mwaka 1950, vikosi vya China viliidhibiti Tibet katika kile ilichokiita ukombozi wa amani na mwaka 1959, Lama alikimbilia India kufuatia kushindwa kwa mapinduzi dhidi ya utawala wa China.

Soma Zaidi: Dalai Lama asisitiza kuwa yuko tayari siku zote kukutana na China.

Blinken anatarajiwa kukutana na waziri mkuu Narendra Modi baadaye hii leo na ataelekea Kuwait baada ya kukamilisha ziara yake ya India.

Mashirika: APE/AFPE/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW