1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Blinken apeleka msukumo wa mapatano Gaza Misri

20 Agosti 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema Israel imekubali pendekezo la kupunguza tofauti zinazokwamisha usitishaji vita na kuachiwa kwa mateka Gaza, na kulitolea wito kundi la Hamas kufanya hivyo pia.

Misri El-Alamein | Kuwasili kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje Antony Blinken baada ya kuwasili El-Alamein, Misri, Agosti 20, 2024.Picha: Kevin Mohatt/REUTERS

Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Antony Blinken alikuwa nchini Misri siku ya Jumanne kwa mazungumzo kuhusu usitishaji vita Gaza baada ya kusema kuwa Israel imekubali pendekezo la Marekani la kuweka madaraja na kuwataka Hamas kufanya vivyo hivyo.

Blinken, katika ziara yake ya tisa Mashariki ya Kati tangu shambulio la wanamgambo wa Kipalestina Oktoba 7 kuanzisha vita na Israel, amesafiri hadi El Alamein, mji wa Mediterania maarufu kwa vita vya Vita vikuu vya vya pili vya Dunia, na kuanza mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah al- Sisi kwenye kasri lake la majira ya kiangazi.

Baada ya hapo, ataelekea kwenye mkutano na Emiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, mjini Doha, eneo la mazungumzo ya kusitisha mapigano wiki iliyopita. Misri na Qatar zote mbili zinafanya kazi pamoja na Marekani ili kupata suluhu katika mgogoro wa Gaza uliodumu kwa miezi 10.

Hata kama Hamas itakubaliana na pendekezo hilo, wapatanishi watatumia muda mwingi katika siku zijazo kufafanua utekelezaji wa makubaliano, alisema Blinken, na kuongeza kuwa bado kuna masuala magumu yanayohitaji maamuzi magumu ya viongozi, bila kutoa ufafanuzi.

Soma pia:Blinken ashinikiza kusitishwa mapigano Gaza 

Washington iliwasilisha pendekezo hilo la karibuni wiki iliyopita kwenye mazungumzo mjini Doha. Blinken alisema Jumatatu kwamba alikuwa na "mazungumzo na manufaa! na waziri mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye "alinithibitishia kwamba Israel inakubali pendekezo la muafaka."

Waziri Blinken akisalimia na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Chaim Zach/Israeli Government Press Office/dpa/picture alliance

Kuelekea mazungumzo hayo, Hamas iliwatolea wito wapatanishi kutekeleza mpango uliopendekezwa na Rais Joe Biden mwishoni mwa mwezi Mei, badala ya kufanya mazungumzo zaidi. Vuguvugu hilo lilisema Jumapili kwamba pendekezo la sasa la Marekani "linaitikia tu mashariki ya Netanyahu."

Msukumo nyuma ya jitihada za sasa

Majadiliano hayo yamepata msukumo katika siku za karibuni wakati ambapo wanadiplomasia wakitumai kwamba makubaliano yataizuwia Iran na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, kulipiza kisasi cha mauaji ya viongozi wawili wa juu wa Hamas na Hezbollah, ambayo Iran iliyalaumu kwa Israel.

Hata hivyo, madai ya Israel ya kuwa na udhibiti wa kudumu wa njia za kimkakati za Gaza, ambayo Hamas imeyakataa kwa muda mrefu, yanatishia kukwamisha juhudi za kufikia muafaka.

Soma pia: Blinken asema Sinwar anapaswa kusimamia makubaliano ya amani Gaza

Maafisa walioko karibu na majadiliano wamesema Israel inataka kuendeleza uwepo wa kijeshi katika ukanda mwembama wa amani kwenye mpaka wa Gaza na Misri, ambao inauita Ukanda wa Philadephia, pamoja na eneo ililoliunda ambalo linaitenga Gaza Kaskazini na Kusini, maarufu kama njia ya Netzarim.

Wachambuzi wanaamini usitishaji vita una uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa sasa kutokana na mashinikizo kwa pande tofauti, ikiwemo uwezekano wa mashambulizi ya kutisha ya Iran na washirika wake, kwa namna isiyo kifani.

Ismail Haniyeh azikwa nchini Qatar

01:39

This browser does not support the video element.

Mtaalamu kutoka taasisi ya Chatham House ya nchini Uingereza Nomi Bar-Yaacov, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba anaanimi serikali ya Marekani imepoteza subira na tabia ya mshirika wake Israel.

Soma pia: Mashambulizi ya Israel yawaua takribani 24 mjini Gaza

''Nadhani  Anthony Blinken yuko tayari kumuumbua Netanyahu ikiwa hatakubali, ikiwa ataongeza masharti mapya, ikiwa hatashikamana na pendekezo la usitishaji vita la Biden na pendekezo la azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ikiwa atang'ang'ana juu ya masharti mapya, ambayo anajua Hamas haitaweza, kuyakubali, nadhani hilo ndilo tunalopaswa kuangalia,'' alisema Bar-Yaacov.

Vifo vya Wapalestina vyazidi kuongezeka

Wakati huo huo, idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na vita hivyo inaendelea kupanda, ambapo maafisa wa afya Gaza wameripoti jana kuwa watu waliothibishwa kuuwa imefikia 40,139 kufikia jana Jumatatu, huku idadi ya waliojeruhiwa ikiwa 92,743.

Kwa upande mwingine, shirika la wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa UNRWA, linasema wafanyakazi wa misaada wasiopungua 289, wakiwemo 207 wa shirika hilo wameuawa Gaza, pamoja na wahudumu wa afya 885.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/mashirika
Mhariri1: Chilumba Rashid

Mhariri2: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW