1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken asema "sasa ni wakati" wa kuvimaliza vita vya Gaza

23 Oktoba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema 'sasa ni wakati' wa kuvimaliza vita vya Gaza. Blinken ameyasema haya wakati ambapo Israel ikidai imewauwa makamanda watatu wa Hezbollah katika saa 48 zilizopita

Israel Tel Aviv | Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiondoka Tel Aviv kuelekea Riyadh 23.10.2024Picha: Nathan Howard/AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwenye kituo cha kwanza cha ziara yake katika kanda ya Mashariki ya Kati amesema "sasa ni wakati" wa kuumaliza mzozo wa Gaza, na ni wakati wa Israel kunufaika na ushindi wa jeshi lake.

Soma Pia: Matumaini ya kusitisha mapigano Gaza yanafifia

Antony Blinken amewasili mjini Riyadh, Saudi Arabia siku ya Jumatano na kabla hajaondoka mjini Tel Aviv alitoa ombi la kutaka uimarishwe uhusiano wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na Israel na pia ameitaka Israel iepushe kuongezeka zaidi mvutano kati yake na Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza na waandishi wa Habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion kabla ya kuondoka kwenda Riyadh Oct.23, 2024Picha: Nathan Howard/AP/picture alliance´

Blinken amesema: "Utetezi wetu ni thabiti kwa Israel, linapokuja suala la mashambulizi kutoka Iran na washirika wa Iran lakini pia ni jambo la muhimu sana kwamba Israel ijibu mashambulizi kwa njia ambayo haitaleta hatari ya kuongezeka au kuueneza mzozo katika eneo zima la Mashariki ya Kati."

Israel imeapa kulipiza kisasi kwa Iran kujibu mashambulizi ya makombora ya Oktoba mosi. Kuna wasiwasi kwamba Israel inaweza kuishambulia miundombinu ya mafuta hali itakayosababisha kupanda kwa bei ya mafuta ghafi duniani.

Soma Pia: Blinken ashinikiza kusitishwa mapigano Gaza 

Wakati huo huo Jeshi la Israel limesema limewaua makamanda watatu wa Hezbollah na wapiganaji wapatao 70 kusini mwa Lebanon katika saa 48 zilizopita, ikiwa ni siku moja baada ya Israel kuthibitisha kumuua Hashem Safieddine, kiongozi aliyeonekana kuwa ndiye mrithi wa Hassan Nasrallah katika kundi hilo la wanamgambo wa Hezbollah. Na leo hii Jeshi la Israel limewaamuru Walebanon zaidi kuondoka kutoka kwenye mji wa bandari wa Tyre.

Katikati: Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hashim Safieddine aliyeuawawa. Alipangiwa kumrithi Hassan NasrallahPicha: Abd Rabbo Ammar/ABACA/picture alliance

Wasiwasi juu ya mgogoro unaoongezeka katika Mashariki ya Kati umesababisha mashirika ya ndege ya kimataifa kuendelea kusimamisha safari zake za ndege kwenda kwenye eneo hilo na pia ndege za mashirika hayo kuepuka kuruka kwenye anga za eneo hilo.

Soma Pia:  Netanyahu: Hakuna eneo tusiloweza kulilenga Mashariki ya Kati

Shirika la ndege la Ujerumani,  Lufthansa limesema Jumatano limesimamisha safari zake za ndege kwenda na kutoka Beirut hadi mwisho wa mwezi wa Februari mwaka ujao kutokana na mapigano makali kati ya Israel na Hezbollah nchini Lebanon. Safari za ndege Kwenda mjini Tel Aviv pia zimesitishwa hadi Novemba 10.

Vyanzo: AFP/AP/ RTRE