1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Blinken awasili China kupunguza joto la mivutano

Sylvia Mwehozi
18 Juni 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewasili mjini Beijing siku ya Jumapili (18.06.2023) na kuanza mazungumzo na waziri mwenzake Qin Gang, yakilenga kupunguza joto la mivutano.

Peking Antony Blinken
Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa MarekaniPicha: Leah Millis/REUTERS

Blinken anakuwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani kuzuru China katika kipindi cha takribani miaka mitano, katikati mwa mahusiano yaliyodorora na matumaini hafifu ya kupatikana mafanikio kwenye orodha ndefu ya mizozo baina ya mataifa hayo tajiri duniani.

Pande zote mbili zimeelezea matumaini ya kuboresha mawasiliano na kuzuia mizozo tofauti kuanzia masuala ya biashara, teknolojia hadi usalama wa kikanda.

Blinken na ujumbe wake wameanza ziara ya siku mbili kwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gang mjini Beijing. Qin na Blinken walitembea kwenye zuria jekundu na kusalimiana kwa kupeana mikono. Awali, Blinken alinukuliwa akisema kuwa atakuwa akitafuta kuepusha "kutoelewana" na "kusimamia vyema" uhusiano na nchi inayotambuliwa na watunga sera wa Washington kama mshindani mkubwa wa Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken katika mkutano na mwenzake wa China Qin Gang.Picha: LEAH MILLIS/REUTERS

Kuelekea ziara hiyo, msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin alieleza kwamba Washington inahitaji "kuheshimu masuala ya msingi ya China" na kuondokana na fikra za kuishughulikia Beijing kimabavu.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken atasafiri kuelekea China.

Afisa mwingine katika wizara ya mambo ya kigeni ya China, aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba "ana matumaini mkutano huo utasaidia kurejesha mahusiano ya Marekani na China kulingana na vile walivyokubaliana marais wa nchi hizo mbili huko mjini Bali, Indonesia.

Matumaini hafifu ya kupiga hatua

Ziara hiyo ilikuwa imeahirishwa tangu mwezi Februari baada ya kutokea sakata la urushwaji wa puto la China linaloshukiwa kuwa la kijasusi katika anga ya Marekani.

Blinken ambaye atasalia nchini humo hadi siku ya Jumatatu, ana uwezekano wa kukutana na Rais Xi Jinping. Tangu wiki iliyopita, maafisa wa Marekani walikuwa na matumaini kidogo ya kupatikana mafanikio wakati wa ziara hiyo, lakini lengo la msingi la Blinken lilikuwa na kuanzisha mawasiliano ya wazi na ya kudumu ili kuhakikisha kwamba ushindani wa kimkakati baina ya nchi hizo haugeuki kuwa migogoro.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken katika mkutano na mwenzake wa China Qin Gang.Picha: LEAH MILLIS/REUTERS

Maafisa wa Marekani na wachambuzi wanatarajia ziara ya Blinken itapisha njia kwa mikutano zaidi baina ya Washington na Beijing katika miezi ijayo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa ziara ya waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen na yule wa Biashara Gina Raimond.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili kuhusu sakata la puto la mwezi Februari, Rais Joe Biden alisema hafikirii uongozi wa China unafahamu mengi kuhusu mahali puto hilo lilipokuwa na lilifanya nini wakati huo akiongeza kuwa anatumai atakutana na Rais Xi hivi karibuni.

Soma pia: Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na China wafanya mazungumzo ya simu

Biden na Xi walikutana ana kwa ana kwa mazungumzo kando ya mkutano wa kilele wa Kundi la nchi za G20 mnamo mwezi Novemba kwenye kisiwa cha Indonesia cha Bali, wakishiriki katika mazungumzo ambayo hayakuwa na mafanikio kuhusu Taiwan na Korea Kaskazini lakini pia kuahidi mawasiliano ya mara kwa mara zaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW