Blinken awasili Misri katika ziara yake ya Mashariki ya Kati
6 Februari 2024Blinken na Sissi pia wataangazia makubaliano ya kubadilisha mateka yaliyoaratibiwa na Misri na Qatar.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani aliondoka mjini Riyadh muda mapema hii leo akitarajiwa kuzuru Qatar na Misri kabla ya kuelekea nchini Israel kujadiliana juu ya makubaliano ya kubadilishana mateka, mipango ya baada ya vita, matarajio ya mataifa ya Kiarabu pamoja na namna Israel itakavyorejesha uhusiano na mataifa hayo.
Ziara hii ya tano ya Blinken kwenye ukanda huo tangu kulipozuka vita kati ya Israel na Hamas mapema mwezi Oktoba, inafanyika wakati Marekani ikiendeleza kampeni yake ya kuishambulia kwa maneno makali wanamgambo wenye mafungamano na Iran, ambao waliwashambulia mwezi uliopita na kuwauwa wanajeshi wake katika kambi ya kijeshi iliyoko Jordan.
Taarifa zinasema, Blinken tayari amekwishawasili mjini Cairo na huko atakutana na viongozi wa Misri ambao kulingana na maafisa wa Marekani watajikita katika makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza ili badala yake mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas waachiliwe huru.
Ziara yake pia inafanyika katikatika ya wasiwasi unaozidi kuongezeka nchini Misri kuhusiana na nia ya Israel ya kuvipanua vita vyake huko Ukanda wa Gaza hadi kwenye maeneo ya mpaka na Misri yaliyofurika watu wa Palestina walioyakimbia makazi yao.
Waziri wa Ulinzi wa Israel alisema mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wao hatimaye yataufikia mji wa Rafah uliopo kwenye mpaka huo na ambako nusu ya watu wa Gaza wanajihifadhi.
Misri tayari imeonya kwamba wanajeshi wa Israel waliopelekwa kwenye mpaka wao wanaweza kutishia makubaliano ya amani yaliyosainiwa na mataifa hayo mawili miongo minne iliyopita. Misri aidha inahofia kuongezeka kwa mashambulizi na kufikia eneo la Rafah, ikisema hatua hiyo itaawafanya Wapalestina wanaoishi kwenye eneo hilo tena katika mazingira magumu kuvuka mpaka na kuingia Misri, kitu ambacho Cairo inasema inataka kukizuia kwa namna ya yoyote ile.
Blinken anaenda Misri baada ya kukutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, na baadae atakwenfa Doha ambako atakutana na Amir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani. Anatarajiwa kukutana pia na Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Mohammed bin Abdulrahman Al Thani.
Umoja wa Mataifa washinikiza pande zinazohasimiana kujizuia ili kuepusha janga zaidi
Afisa wa ngazi za juu kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya siasa na amani Rosemary DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo mjini New York kuendelea kuzishinikiza pande zinazohasimiana kujizuia ili kuepusha mzozo uliopo kusambaa zaidi.
"Ninatoa wito kwa Baraza kuendelea kushirikiana kikamilifu na pande zote zinazohusika ili kuzuia kuongezeka zaidi na hali mbaya ya mvutano inayodhoofisha amani na usalama wa kikanda."
Mamia ya watu wameuawa katika siku za karibuni wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake kuelekea mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis wakati watu idadi jumla ya watu wa Gaza wapatao milioni 2.3 wakikabiliwa na hali mbaya kutokana na ukosefu wa chakula, miongoni mwao watu 576,000 wakikabiliwa na kitisho cha njaa.
Kulingana na Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas kwenye Ukanda wa Gaza, karibu watu 27,585 wameuawa katika vita hivyo. Idadi hii ya sasa inahusisha watu 107 waliouawa masaa 24 yaliyopita, imesema wizara hiyo, huku wengine 66,978 wakiwa wamejeruhiwa vibaya.
Jeshi la Israel limesema limewaua magaidi kadhaa tangu jana na karibu watu 80 wanaotuhumiwa kujihusisha na shughuli za kigaidi wamekamatwa, ikiwa ni pamoja na magaidi walioshiriki kwenye shambulizi la Oktoba 7. Taarifa yake imeongeza kuwa wanajeshi wake aidha wamewaua zaidi ya wanamgambo 15 na meli ya kijeshi pia ilishambulia kile ilichoita maficho ya magaidi.
Mwandishi wa habari wa shirika la AFP amearifu kwamba raia wanahaha, wakitafuta mahala salama pa kukimbilia na hasa kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi huko Khan Younis na kufuatia kitisho cha kufikia sasa kwenye eneo la Rafah.