Blinken azungumza na Makamu wa Rais wa China Han Zheng
19 Septemba 2023Mkutano wao ni sehemu ya mfululizo wa mashauriano ya ngazi ya juu baina ya nchi hizo mbili inayolenga kupunguza mivutano.
Mazungumzo kati ya Blinken na Zheng yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yanaweza kusaidia kufungua njia ya kuandaliwa kwa mkutano kati ya rais Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping mnamo majira ya mapukutiko.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Blinken amesema ulimwengu una shauku ya kuona China na Marekani zinashughulikia mahusiano yao na "njia pekee ya kufanya hivyo ni kupitia diplomasia ya ana kwa ana".
Mazungumzo hayo yanafuata mengine kadhaa ya miezi ya karibuni kati ya maafisa wa Marekani na China yaliyokuwa na lengo la kuimarisha mahusiano yalipwaya kutokana na mivutano ya kimtazamo na maslahi baina ya nchi hizo mbili.