Blinken azungumza na rais Kagame
6 Desemba 2022Hayo yametangazwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani jana Jumatatu ambayo pia ilisema Blinken alizungumzia wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa umwagaji damu.
Msemaji wa wizara hiyo Ned Price ameeleza kwamba Blinken alizungumza kwa njia ya simu Jumapili na kiongozi huyo wa Rwanda na kuweka wazi kwamba hatua yoyote ya nje ya kuyaunga mkono makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inapaswa kusitishwa, ikiwemo uungaji mkono kutoka Rwanda kwa kundi la M23.
Blinken pia amelaani kuzuka tena kwa matamshi ya chuki na kauli za uchochezi zinazotolewa hadharani zikiilenga Rwanda na kukumbusha athari za kutisha za kauli kama hizo, zilizoshuhudiwa mwaka 1994 katika vita vya kimbari vilivyowalenga watu jamii ya kabila la Watutsi.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani amezitolea mwito Kongo na Rwanda kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi uliopita nchini Angola.