1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Blinken: Tutaendelea kuikabili Urusi inapoishambulia Ukraine

12 Septemba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema, nchi yake itaendelea kuikabili Urusi inapoishambulia Ukraine kadri hali inavyobadilika.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi habari na mwenzake wa Poland Zbiegniew Rau huko Rzeszow, Poland, mnamo Machi 5, 2022.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Olivier Douliery/AP/picture alliance

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari mjini Warsaw na mwenzake wa Poland, Radoslaw Sikorski, Blinken aliacha uwezekano wa usafirishaji zaidi wa silaha nchini Ukraine.

Soma pia:Marekani, UK zaahidi jibu la haraka kwa maombi ya Ukraine

Blinken amesema mojawapo ya madhumuni ya ziara yake nchini Ukraine hapo jana ilikuwa ni kusikia kutoka kwa washirika wao wa nchi hiyo kuhusu wanachoamini kuwa wanahitaji hivi sasa ili kukabiliana vyema katika uwanja wa vita nchini humo.

Poland yasema tayari Iran inakabiliwa na vikwazo vikali

Wakati wa mkutano huo na waandishi habari, Sirkorski alipoulizwa ikiwa Poland mshirika mkubwa wa Ukraine itavunja uhusiano na Iran, inayodaiwa kusafirisha makombora ya masafa mafupi hadiUrusi, alisema kuwa tatizo la Poland ni kwamba Iran tayari inakabiliwa na vikwazo vikali na kwamba haoni kama kuna la zaidi linaloweza kufanywa na Poland.

Soma pia:Mawaziri Blinken na Lammy waapa kuisaidia zaidi Ukraine

Wiki hii, mataifa ya Magharibi yenye nguvu yaliweka vikwazo vipya vinavyoilenga sekta ya usafiri wa anga ya Iran ikiwa ni pamoja na shirika la ndege la Iran huku Ukraine ikionya kuwa huenda ikakata uhusiano na Tehran.

Waziri wa mambo ya nje wa Poland Radoslaw SikorskiPicha: Marek Antoni Iwanczuk/picture alliance

Blinken alikuwa akihitimisha ziara ya mataifa matatu ya Ulaya inayolenga Ukraine nchini Poland baada ya kusikiliza maombi ya mara kwa mara kutoka kwa maafisa wa Ukraine kutumia silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kwa mashambulizi ya masafa marefu ndani ya Urusi.

Iran yawaita mabalozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi

Serikali ya Iran leo imewaita mabalozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi kuhusiana na madai yao kwamba Tehran ilisambaza makombora ya masafa mafupi kwa Urusi kuyatumia dhidi ya Ukraine.

Shirika la habari la serikali IRNA, limeripoti kuwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo iliwaita mabalozi hao kando kando hii leo kushtumu vikali madai hayo.

Shambulizi la Urusi lalenga meli ya nafaka katika Bahari Nyeusi

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andrii Sybiha, amesema leo kuwa shambulizi la Urusi dhidi ya meli inayobeba nafaka katika Bahari Nyeusi lilikuwa shambulizi la wazi dhidi ya uhuru wa urambazaji na usalama wa chakula duniani.

Awali, maafisa nchini Ukraine walisema kuwa meli ya mizigo iliyokuwa imebeba nafaka kutoka Ukraine ililengwa na kombora la Urusi katika eneo la kiuchumi la bahari ya Romania.