1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken ziarani Afrika kudumisha ushawishi wa Marekani

Saleh Mwanamilongo
23 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alithibitisha azma ya Marekani kuimarisha uhusiano na Afrika kwa kuanza ziara yake nchini Cape Verde.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akutana na Waziri Mkuu wa Cape Verde José Ulisses
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akutana na Waziri Mkuu wa Cape Verde José UlissesPicha: Ângelo Semedo/DW

Blinken alianzia ziara yake huko Cape Verde hapo jana kabla ya kuelekea Ivory Coast ambako aliwasili mchana. Aliposhuka kwenye ndege, alikwenda moja kwa moja kwenye uwanja wa Abidjan kutazama mechi kati ya Ivory Coast, mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, ambayo ililazwa na Equatorial Guinea magoli 4 kwa 0. Blinken baadae atasafiri hadi Nigeria na Angola.

Wenyeji wake huko Abidjan walitoa jezi yenye jina lake kwa Blinken, shabiki wa soka, ambaye alisema mchezo ulikuwa njia nyingine ya kujenga uhusiano kati ya Marekani na Afrika. Kwenye visiwa vya Cape Verde vyenye wakaazi laki tano, Blinken alisema nchi hiyo ni mfano wa utulivu na iliopiga hatua katika kuimarisha demokrasia.

"Marekani imejitolea kuimarisha, na kutoa ushirikiano wake barani Afrika, ushirikiano ambao unanufaisha Waafrika na Wamarekani. Kama vile Rais Biden alivyosema, sote tunajihusisha na Afrika.'' alisema Blinken.

Kabla ya kuendelea kusema : ''Lakini lazima niwaambie, kuna sababu nzuri kwamba tunaanzia hapa Cape Verde, na hiyo ni kwa sababu ni mshirika wa mzuri wa Marekani. Na kama ulivyosema, Waziri Mkuu, huu ni ushirikiano ambao kimsingi unazingatia maadili ya pamoja, maslahi ya pamoja, na pia historia ya kina ya pamoja'', alisema Blinken. 

Marekani kuongeza uwekezaji wake barani Afrika

China imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu katika bara la Afrika, hasa kufadhili miundombinu katika nchi nyingiPicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Mzozo wa Ukraine na uungaji mkono wa Marekani kwa serikali ya Kyiv dhidi ya Moscow umezigawanya nchi za Kiafrika. Waziri Mkuu wa Cape Verde Ulisses Correia e Silva alisema nchi yake inalaani vikali uvamizi wa Urusi. Pia alikosoa mapinduzi ambayo Afrika imepitia katika miaka ya hivi karibuni, na akathibitisha kwamba Cape Verde iliongozwa na maadili ya demokrasia huria.

Marekani imetoa kiasi cha dola milioni 150 kwa Cape Verde kupitia programu mbili, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa bandari katika mji mkuu Praia, uboreshaji wa barabara na mfumo wa usambazaji maji ya kunywa.

Ushawishi wa Marekani dhidi ya Urusi na China ?

China imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu katika bara la Afrika, hasa kufadhili miundombinu katika nchi nyingi.  Kwa upande wake, Urusi imeendeleza ushawishi wake katika nchi kadhaa za Kiafrika zinazozungumza Kifaransa katika miaka ya hivi karibuni, hasa kwa uwepo wa kundi la wanamgambo wa Wagner katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali na uhusiano na Burkina Faso.

Utawala wa Biden ulitangaza mwaka jana mpango wa miaka kumi wa kuhimiza utulivu na kuepuka migogoro katika nchi za Benin, Ghana, Guinea, Ivory Coast na Togo, nchi za pwani ambazo zinatishiwa pia na makundi ya kigaidi.