Boateng kuwa nahodha mpya wa Ujerumani?
1 Agosti 2016Wakati Ujerumani inaangalia mustakabali wake, Michael da Silva anaelezea ni kwa nini timu hiyo sasa inahitaji nahodha atakayeiwakilisha jamii ya tamaduni tofauti. Taarifa kwamba Bastian Schweinsteiger ameamua kuacha kuichezea timu yake ya taifa, inaleta ujumbe wa mwisho wa zama za mmoja wa wachezaji muhimu aliyepewa sifa katika timu ya taifa ya Ujerumani.
Huku akiwa na majeraha, Schweinsteiger alifanikiwa kuipeleka Ujerumani katika kipindi cha ziada wakati wa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Argentina, mwaka 2014 katika mtindo wa kishujaa.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Philipp Lahm, Per Mertesacker na Miroslav Klose, kabla yake, Schweinsteiger amekuwa sehemu ya manahodha wa zamani na sasa Ujerumani inapaswa kuangalia mustakabali wake.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Löw, ambaye hivi karibuni alielezea nia yake ya kuendelea na timu hiyo hadi ifikapo angalau mwaka 2018, anahitaji mtu mpya wa kuiongoza timu ya Ujerumani ambayo tayari inaonekana iko tofauti na ile iliyojipatia ushindi katika michuano ya Rio de Janeiro. Michuano ya kombe la dunia itakayofanyika Urusi mwaka 2018, ndiyo lengo lijalo na Löw anahitaji kupata msukumo mpya.
Je nani atavivaa viatu vya Schweinsteiger?
Ni wazi kuna majina matatu: Manuel Neuer, Sami Khedira na Jerome Boateng, huku Mats Hummels akiwa pia anatajwa. Wote hao wana haiba ya uongozi na wana nafasi ya kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani, lakini hakuna hata mmoja wao mwenye nafasi zaidi ya Boateng. Mchezaji huyo wa Bayern Munich, amekuwa mlinzi mwenye hadhi ya kimataifa ndani Bayern Munich na pia kuna sababu ya kumuita mwamba.
Mchezo wake uliimarika chini ya Pep Guardiola katika uwanja wa Bayern Munich wa Allianz Arena na katika kiwango cha kimataifa yeye ni msingi wa mbinu za mchezo za kocha Löw, mwenye uwezo wa kucheza na mpira lakini vile vile ni mlinzi asiyeshindika na anayeonyesha mfano kwenye timu nzima. Ni mtu aliyebobea na jasiri, mwenye msukumo lakini mnyenyekevu, Boateng ana sifa zote ambazo Löw anazihitaji katika kumchagua kiongozi.
Lakini kuangalia zaidi mchango wake muhimu akiwa uwanjani, uteuzi wa Boateng unaweza kuwa kauli sio tu kwenye timu, lakini Ujerumani kwa ujumla. Khedira na Neuer pia ni chaguo bora na uamuzi wa kumteua Boateng kuwa nahodha hautokuwa wa moja kwa moja. Kuumia kwake na kupewa kadi nyekundu mara kwa mara, ni vizingiti dhidi yake.
Boateng hawawakilishi tu Waafrika 235,000 wanaoishi Ujerumani, lakini utamaduni wa taifa uliokubaliwa na watu wote. Uamuzi wa kumteua Boateng pia utakuwa muhimu dhidi ya kauli iliyotolewa na msemaji wa chama mbadala kwa Ujerumani AfD, kinachopinga wahamiaji, Alexander Gauland, aliyenukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine akisema: ''watu kama Boateng wanaheshimika kama wachezaji, lakini wajerumani hawamuhitaji Boateng kama jirani yao.
Mwandishi: Michael da Silva
Tafsiri: Grace Patricia Kabogo/DW http://bit.ly/2aroQ8Z
Mhariri: Daniel Gakuba