BoB 2012: Blogu ya Kiirani yashinda
2 Mei 2012Kwa hakika "Dirisha la Hofu" linavitonesha vidonda vya Iran, lakini Arash Sigarchi anaweza kuyafanya hayo kutokea nje ya Iran. Katika blogu yake, Sigarschi anasema "ni kashfa kubwa" ni "fedheha mara mbili" kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Anapigia mfano wa mkasa wa afisa wa kidiplomasia wa ngazi za juu wa Iran aliyemnyanyasa kingono mtoto wa kiume nchini Brazil. Taarifa juu ya kashfa hiyo ilichapishwa kwa kina katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, lakini ubalozi wa Iran ulijaribu kuzipuuza taarifa hizo na kusema kuwa ni matokeo ya kutoelewana kitamaduni. Taarifa kama hizo hazichapishwi katika vyombo vya habari vya Iran au hata vikichapishwa, zinapotoshwa.
Sigarchi anasema utawala wa Iran unajifanya kuwa na uadilifu wa kuyafuata maagizo ya dini, ambapo kwa utawala huo uhusiano wa mapenzi nje ya ndoa, yaani zinaa, ni dhambi. Lakini sasa limeripuka bomu dhidi ya utawala huo kwani mwakilishi wake wa kibalozi amemnyanyasa kingono mtoto mdogo wa kiume. Adhabu ya udhalimu huo ni kifungo cha miaka 14 jela.
Yasiyofanywa Iran, yafanywa kwenye "Dirisha la Hofu"
Wakati vyombo rasmi vya Iran havichapishi taarifa kama hizo, blogu ya "Dirisha la Hofu" aliyoianzisha Sigarchi mnamo mwaka wa 2008 akiwa ukimbizini mjini Washington inafanya hivyo.
Miaka minne kabla ya hapo, wakati bado angali nchini Iran, Sigarchi alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kuandika maneno ya kukosoa kama mwandishi. Hata hivyo kutokana na bidii ya wakili wake, Shirin Ebadi mshindi wa nishani ya amani ya Nobel, adhabu ya Sigarchi ilipunguzwa hadi miaka mitatu.
Lakini baada ya hapo mwandishi habari huyo alianza kuandamwa na mikosi. Ndugu yake Ashkan alikufa katika ajali ya gari. Yeye mwenyewe alipata maradhi ya saratani wakati akiwa kifungoni. Lakini hakushika tama.
Miongoni mwa waliokuwamo kwenye jopo la majaji ya Blogu Bora, Arash Abadpour, ambaye pia anatoka Iran, amesema kuwa Sigarchi hakupoteza dira na licha ya mikosi iliyomwandama, mwandishi huyo ameendelea kuwa imara.
Wapinzani wengine wa utawala wa Iran wamedai kwamba Sigarchi anaandika taarifa zenye mwelekeo wa kuiridhisha serikali, lakini Sigarchi anatumia hoja, akisema kuwa yeye ni mwandishi wa habari na anachokiandika kina uzito kwa mtazamo wa kiuandishi.
Mwandishi huyo alichaguliwa na jopo la kimataifa la waamuzi 12 kwenye makao ya Deutsche Welle jijini Berlin. Mhariri Mkuu wa Deustche Welle, Ute Schaeffer, amesema DW ni Umoja wa Mataifa wa Blogu na miradi ya tovuti
Ute Schaeffer amesema Deutsche Welle imejenga jina zuri duniani kote kutokana na kuandaa mashindano haya ya Blogu Bora.
Mwandishi: Aya Bach
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman