1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine aidhinishwa kugombea urais Uganda

3 Novemba 2020

Tume ya uchaguzi Uganda hatimaye imemteua mwanamuziki maarufu aliegeuka mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu Bobi Wine, kuwa mgombea rasmi wa urais katika uchaguzi mkuuu utakaofanyika mapema mwakani

Robert Kyagulanyi
Picha: Emmanuel Lubega/DW

Kyagulanyi ameibuka kuwa hasimu mkuu wa kisiasa wa rais wa muda mrefu wa taifa hilo Yoweri Museveni, lakini uteuzi wake hii leo umekumbana na mkono wa chuma wa jeshi polisi, baada ya kukamatwa na polisi na polisi, na wauasi wake kukabiliana na vikosi vya usalama wakati wakishangilia uteuzi wake. Mgombea mwingine amewasilisha nyaraka zake akiwa miguu tupu baada ya kuhujumiwa na polisi. 

Huyo ndiye mwanasiasa na msanii Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine akiwaongoza wafuasi wake wachache waliomsindikiza kuteuliwa na tume huru ya uchaguzi. Akizungumza mara baada ya uteuzi wake, Bobi Wine amesema anawania nafasi hiyo ya juu kabisaa nchini Uganda ili kuwawakilisha watu wanaokandamizwa, walio dhaifu, maskini na wenye kudhulumiwa mingoni mwa wengine "Natumia wakati huu kutangaza kwamba tunachoshuhudia sasa ni uzinduzi wa awamu muhimu katika mapambano yetu ya kuikomboa nchi yetu kutoka kwenye minyororo ya udikteta uliotukwamisha kwa karibu miongo minne. Tumevifunga vitabu vya malalamiko. Sasa tumefungua kitabu cha vitendo. Niko hapa kumnusuru rais Museveni kutokana na yeye mwenyewe; kutokana na rushwa yake na ulezi wake miongoni mwa mengine.

Bobi Wine alikamatwa muda mfupi baada ya kuidhinishwaPicha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture-alliance

Bobi Wine amepata umaarufu mkubwa miongoni mwa tabaka la vijana katika taifa ambako wastani wa umri ni miaka 16. Tangu kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2017, amekuwa akikamatwa mara kwa mara na kuweka katika kifungu cha nyumbani, kupigwa marufuku kwa maonesho yake na mikutano yake ya umma imekuwa ikisambaratishwa kwa mabomu ya kutoa machozi.

Kabla ya uteuzi wake, wafuasi wake walikuwa na wasiwasi kwamba lolote lingefanyika asiweze kufanikisha azma hiyo, kutokana hasa na masharti makali ya tume ya uchaguzi kuhusiana na kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19, lakini zaidi kutokana nahatua ya vyombo vya usalama kuzingira nyumba yake usiku kucha. Makamu wa rais wa chama cha NUP Mashariki mwa Uganda John Baptist Nambeshe amesema.

Wagombea wengine katika kinyang'anyiro hicho pia walikumbwa na mashaka walipokuwa wakifanya maandalizi ya kwenda kuteuliwa kwa wakati waliopangiwa. Kwa mfano, mshika bendera wa chama kikuu cha upinzani FDC Patrick Oboi Amuriat alifikishwa miguu tupu kwenye kituo cha uteuzi na maafisa wa polisi waliomkamata akijaribu kuingia katika ofisi yake kuchukua nyaraka zake za uteuzi.

Mgombea mwenye umri wa chini kabisa katika kinyang'anyiro hiki ni kijana John Katumba mwenye umri wa miaka 25 aliyehitimu elimu yake ya chuo kikuu hivi karibuni. Hii ina maana anawania kiti hicho dhidi ya rais Museveni anayemzidi kwa zaidi ya miaka 50. Alipokuwa akizindua ilani yake ya uchaguzi baada ya kuteuliwa, rais Museveni alidokeza kuwa si nia na kwa maslahi yake binafsi kung'ang'ania madarakani ila kuweza kutimiza ndoto iliyotawala maisha ya wazalendo wa Afrika akina Mwalimu Nyerere, Nkrumah, Kenyatta na Kaunda ya kujenga shirikisho la kisiasa katika bara hilo.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.