Bobi Wine akamatwa tena na Polisi
31 Agosti 2018Duru za habari zimearifu kuwa Kyagulanyi alizuiwa na kisha kukamatwa na maafisa wa polisi katika uwanja wa ndege wa Entebbe muda mfupi kabla ya kuabiri ndege kuelekea Marekani na kulingana na wakili wa mbunge huyo polisi haikutoa maelezo yoyote ya juu ya hatua hiyo.
Polisi ilisema baadae kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa wamemzuia mbunge huyo kwa sababu za usalama kwa kuwa mbunge huyo yuko nje kwa dhamana pekee na kuongeza kuwa inasubiri maelekezo kutoka idara za serikali zinazohusika.
Tangu wakati huo mwanasiasa huyo amezuiliwa katika hospitali moja ya serikali mjini Kampala na polisi imesema atapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa polisi.
Mke wa Kyagulanyi, Barbara, aliandika kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa maafisa wa usalama walimchukua kwa nguvu mumewe ambaye alikuwa akilalamika kwa maumivu na kupaza sauti ya kuomba msaada.
Dhamana yake haimzuii kusafiri nje
Wakili wake Nicholas Opiyo amesema kushikiliwa kwake ni kinyume cha utaratibu na amezituhumu mamlaka nchini Uganda kwa kujaribu kutengeneza taarifa zao wenyewe juu ya afya ya Bobi wine ili kuficha ushahidi wa mateso na majeraha aliyopata.
Opiyo ameonya kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa daktari yeyote atakayemtibu mwanamuziki huyo bila ridhaa yake atakuwa amekiuka kiapo na atakabiliwa binafsi kwa mujibu wa sheria.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 36 aliachiwa kwa dhamana siku ya Jumatatu bila ya kuwekewa zuio lolote la kutosafiri ambapo Mahakama pia iliamuru kutozuiliwa kwa hati yake ya kusafiria
Bobi Wine ni miongoni mwa kundi la wabunge watano waliokamatwa katikati ya mwezi Agosti katika mji wa kaskazini-magharibi wa Arua kwa tuhuma za kushambulia kwa mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa mkuano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa ubunge.
Wakili wa mbunge huyo ameyaita madai huyo kuwa ya uongo na uzushi.
Ukosoaji juu ya anavyotendewa ni mkubwa
Madai kuwa Bobi Wine na wenzake walitesewa yalizusha maandamano makubwa kwenye mji mkuu Kampala na maeneo mengine ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Wiki iliyopita wanamuziki kadhaa mashuhuri ulimwenguni akiwemo Chris Martin, Angelique Kidjo na Brian Eno walichapisha barua ya wazi kulaani jinsi Bobi wine alivyotendewa ambaye alipoonekana kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa alitembea kwa kutumia magongo huku akitokwa machozi.
Bobi Wine ambaye alishinda kiti cha ubunge kama mgombea binafsi mwaka uliopita ameibuka kuwa mwanasiasa wa upinzani mwenye nguvu na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Yoweri Museveni tangu katiba ilipofanyiwa mabadiliko ili kuondoa ukomo wa umri wa kuwania urais.
Katika hatua nyingine hapo kabla maafisa katika uwanja wa ndege wa Entebbe walimzuia pia mbunge mwengine Francis Zake kusafiri kwenda India wakisema ni mtuhumiwa wa kesi ya jinai.
Mwandishi: Rashid Chilumba/APE/AFPE.
Mhariri: Iddi Ssessanga