Bobi Wine azinduwa maandalizi kuelekea uchaguzi wa 2026
28 Agosti 2023Akiwahutubia watu wa sehemu hiyo, Bobi Wine aliihimiza jamii ya Waankole kuondokana na kasumba kwamba watu wa jamii zingine za Uganda zina uhasama dhidi yao na Yoweri Museveni akiondoka madarakani watalipiza kisasi dhidi yao, akisema hiyo imekuwa mbinu ya Rais Yoweri Museveni kusababisha migawanyiko miongoni kwa raia ili kuendeleza utawala wake.
"Nataka mfahamu kuwa walituvisha hofu. Tumekuwa tukipigana hiyo hofu wakati wote." Alisema mwanamuziki huyo aliyegeuka alama ya siasa za upinzani nchini Uganda.
Soma zaidi: Museveni aadhimisha miaka 37 tangu alipoingia madarakani
Viongozi wa NUP katika eneo hilo waliwataka watu wa jamii nyingine za Uganda wafahamu kuwa watu wa Ankole pia hukumbwa na hali ngumu za maisha licha ya kuwa rais wa sasa anatokea sehemu hiyo, na ndiyo maana nao wanamuunga mkono Bobi Wine alete mageuzi kabambe katika utawala wa Uganda.
"Hamna kazi, hamna dawa hospitalini, barabara zenu zi nzuri na ndivyo hali ilivyo Ankole kama sehemu zingine za nchi. Hatuna kazi, hatuna pesa huu ni wakati wetu sote kujipigania." Alisema mmoja wao.
NUP yaonesha ingali hai
Wafuasi wa chama hicho waliuelezea mkutano huo kuwa kielelezo cha kuondoa madai kwamba chama hicho hakina ufuasi magharibi mwa Uganda.
Hapo awali, palikuwa na mashaka kama mkutano huo ungeruhusiwa kuendelea. Hii ni baada ya kituo cha redio cha Indijitto alichopangiwa kuwasiliana na watu kupitia hewani kuzimwa.
Soma zaidi:Mjadala waibuka kuhusu mageuzi ya katiba nchini Uganda
Aidha, polisi walizingira shule ambako mkutano huo ungefanyika na kuagiza watu wasikusanyike.
Lakini baada ya saa mbili hivi, masharti yalilegezwa na waandazi kuruhusiwa kuendelea na mkutano huo.
Bobi Wine alisisitiza kuwa si mapenzi ya Museveni kukubali mkutano huo kufanyika lakini ni kutokana na shinikizo la watu ndani na nje ya nchi ndipo sasa hana budi kuwaacha waendelee kuwahamasisha wananchi.
Harakati kuelekea 2026
"Hatuko hapa kwa mapenzi ya Museveni. Hakutaka tuwe hapa kuwambia ukweli ndiyo maana redio ilizimwa. Lakini hongereni watu wa Mbarara kwa kutobabaishwa." Alisema.
Viongozi wa chama hicho waliwasifu sana polisi kwa kujidhibiti wenyewe na kuuacha mkutano huo kufanyika kwa amani.
Chama cha NUP kimetangaza kuwa kitaendesha mikutano hiyo kujiimarisha mashinani na kuondoa mashaka miongoni mwa wapiga kura kwamba kimefifia.
Chama hicho kingali kinapinga ushindi wa Rais Museveni mwaka 2021 ulioamuliwa na mahakama ya juu.
Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala