1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine kupasuliwa baada ya kujeruhiwa mguuni

4 Septemba 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine atafanyiwa upasuaji, wakili wake amesema Jumatano, siku moja baa ya kupata jeraha la mguuni katika tukio la vurugu ambamo awali chama chake kilisema alipigwa risasi.

Uganda Kampala | Kiongozi wa upinzani Bobi Wine akiwa hospitalini baada ya kushambuliwa
Kiongozi wa upinzani Bobi Wine akiwa hospitalini baada ya kushambuliwa.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Mkosoaji huyo mkubwa wa Rais Yoweri Museveni alikuwa katika mji wa Bulindo, karibu kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu Kampala, wakati chama chake cha National Unity Platform (NUP) kilisema tukio hilo lilitokea.

Lakini siku ya Jumatano wakili wake, George Musisi, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba Bobi Wine "hayuko hatarini tena lakini kwa mujibu wa madaktari atafanyxiwa upasuaji kuondoa kipande kinachoshukiwa kutoka kwenye bomu la kutoa machozi, lililompiga."

"Inaonekana polisi walilenga kumdhuru," Musisi aliongeza.

Katika hali ya kutatanisha baada ya tukio la Jumanne, kiongozi huyo wa upinzani, amabye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alikimbizwa katika Hospitali ya Nsambya huku picha na video zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha kijana huyo mwenye umri wa miaka 42 akiugulia maumivu.

Musisi alisema tukio hilo lilitokea wakati polisi walipofyatua mabomu ya machozi  hovyo dhidi ya kundi dogo la wafuasi katika mji wa Bulindo, ambapo Wine alikuwa kwenye mkutano. "Bomu la machozi lilimlenga na kulipuka na kumjeruhi mguuni,” alisema.

Polisi imekuwa ikitumia nguvu kubwa kukabiliana na Bobi WIne na wafuasi wake nchini Uganda.Picha: SUMY SADURNI/AFP

Polisi wakosolewa kwa matumizi ya nguvu iliyopitiliza

Musisi alilaani kisa hicho na kusema polisi wamewakamata wafuasi wanne wa chama hicho wakati wa ghasia hizo. Polisi ya Uganda ilisema Jumanne kwamba itafungua uchunguzi kuhusu "tuhuma za kupigwa risasi na matukio yoyote yanayohusiana nalo."

Soma pia:Bobi Wine azinduwa maandalizi kuelekea uchaguzi wa 2026

Taarifa hiyo, iliyochapishwa kwenye X, ilisema maafisa katika eneo la tukio walipinga maelezo ya wapinzani, wakisema Wine alijikwaa na kujijeruhi wakati akiingia kwenye gari lake.

Msemaji wa chama cha NUP alielezea hali hiyo Jumanne jioni, akilaani vitendo vya polisi. "Muda mfupi baada ya yeye kushuka kwenye gari, watu hawa waliokuwa karibu sana walimlenga kwa bomu ambalo liligonga mguu wake wa kushoto," Joel Ssenyonyi aliwaambia waandishi wa habari.

"Amepata jeraha, mfupa ulichubuka lakini nashukuru haukuvunjika," alisema na kueleza kuwa bomu la machozi lilipuka na "vipande" viliingia kwenye mguu wake.

Kwenye mitandao ya kijamii, watu mbalimbali wameelezea kughadhabishwa na tukio hilo, na kuelezea kero na mashaka yao kuhusu kisa cha  Bobi Wine kujeruhiwa katika mazingira ambapo shughuli zake hazikuwa za kisiasa.

Kila aendapo, Bobi huvutia umati mkubwa wa watu na hivyo kuzusha tafrani na polisi.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

"Madaktari wanasema itahitaji upasuaji zaidi ili kutoa vipande hivyo."

Mwiba kwa utawala wa Museveni

Bobi Wine na chama chake cha NUP wamekuwa mwiba kwa Museveni, ambaye ameitawala Uganda kwa takriban miaka 40.

Soma pia: Polisi Uganda yazuwia mapokezi ya Bobi Wine

Aliwabua uraisi dhidi ya Museveni mwaka wa 2021, lakini kiongozi huyo mkongwe alitangazwa mshindi kwa muhula wa sita.

Upinzani ulilaani kura hiyo na kusema kuitaja kuwa ya udanganyifu, kufuatia kampeni iliyoambatana na vitisho, kukamatwa kwa upinzani na ghasia.

Wine amekuwa akizuiliwa mara kadhaa na mikutano ya hadhara na chama chake imetawanywa kwa fujo.

Adui wa Museveni ni Museveni mwenyewe - Bobi Wine

06:34

This browser does not support the video element.

Chanzo: Mashirika