Boeing yakabiliwa na kesi ya madai ya ajali ya ndege 737 MAX
5 Mei 2026
Kampuni kubwa ya kutengeneza ndege ya Marekani Boeing imerejea mahakamani Jumatatu kukabiliana na kesi dhidi yake ya hivi punde kuhusu ajali mbaya ya ndege aina ya Boeng 737 MAX nchini Ethiopia, iliyofunguliwa na familia ya mfanyakazi kijana Samya Stumo wa asasi isiyo ya kiserikali ya Marekani, ThinkWell.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuwasilishwa katika mahakama ya shirikisho huko Chicago, huku uteuzi wa majaji ukitarajiwa kufanyika jana Jumatatu na leo Jumanne na taarifa za ufunguzi hapo kesho Jumatano.
Samya aliuawa katika ajali ya ndege ya shirika la Ethiopian Airlines mnamo Machi 2019, alipokuwa njiani kuelekea Kenya kwa kazi yake ya kwanza na asasi ya ThinkWell, shirika lisilo la kiserikali la afya ya umma lililolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika na Asia.
Lakini ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Addis Ababa, na kumuua kila mtu aliyekuwa ndani.
Ajali hiyo ya Ethiopia ilifuatia ajali ya ndege ya Lion Air yapata miezi minne na nusu kabla huko nchini Indonesia. Ajali hizo mbili zilisababisha vifo vya watu 346 kwa jumla.
Boeing ilikiri kwamba programu za kuzuia kusimama zilihusika katika ajali zote mbili.