1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram limewaachilia huru wasichana 21 waliotekwa nyara

13 Oktoba 2016

Hili ni kundi la kwanza la wasichana hao kuachiliwa kufuatia mazungumzo kati ya serikali na kundi hilo. Mazungumzo yaliyoongozwa na kamati ya kimataifa ya shirika la Msalaba Mwekundu, pamoja na serikali ya Uswizi.

Screenshot mutmaßliches Boko Haram Video
Picha: youtube/Fgghhfc Ffhjjj

Kundi la kigaidi la Boko Haram limewaachilia huru wasichana 21 waliotekwa nyara. Wasichana hao ambao ni miongoni mwa 276 waliotekwa nyara zaidi ya miaka miwili iliyopita, wameachiliwa baada ya wafungwa wanne wa kundi hilo pia kuachiliwa huru na serikali. Serikali ya Nigeria imesema hayo yote ni kutokana na mazungumzo kati ya serikali na Boko Haram. Hata hivyo hatma ya wasichana wengine 197 bado haijulikani.

Wasichana walioachiliwa, wapo chini ya ulinzi wa wizara ya huduma za nchi, na shirika la ujasusi wa nchi hiyo. Baadaye watawapelekwa kwa makamu wa rais Yemi Obinsajo, kwa kuwa rais Muhammadu Buhari yupo ziarani Ujerumani. Hayo yamesemwa na msemaji wa rais Garba Shehu.

Hili ni kundi la kwanza la wasichana hao kuachiliwa kufuatia mazungumzo kati ya serikali na kundi hilo. Mazungumzo yaliyoongozwa na kamati ya kimataifa ya shirika la Msalaba Mwekundu, pamoja na serikali ya Uswizi. Japo amesema kuwa mazungumzo zaidi yanaendelea kuhakikisha wasichana wengine ambao wangali wanatekwa nyara pia wanaachiliwa huru, haijajulikana wazi ni wangapi miongoni mwao huenda wameaga dunia. Katika video moja linaloonyesha baadhi ya wasichana waliotekwa nyara, mmoja anayeulizwa maswali na mwanachama wa Boko Haram anaisihi serikali ya Nigeria kushughulika ili wao pia waachilie huru.

Mwanajeshi mmoja anayefahamu mazungumzo hayo lakini hakutaka kutambulishwa jina, amesema wasichana hao waliachiliwa kwa njia ya kubadilishana na wafungwa wanne wa kundi hilo walioachiliwa huru na serikali ya Nigeria usiku wa kuamkia Alhamisi mjini Banki kaskazini mashariki ya mpaka wa Cameroon. Amesema kuwa wasichana hao 21 walisafirishwa kwa helikopta hadi Maidiguri.

Mwanamke akipita karibu na wanajeshi wa Nigeria katika kizuizi cha GwozaPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Oyekanmi

Kundi la wanaharakati ambalo limekuwa likiendeleza kampeni ya kutaka wasichana hao kuachiliwa huru kupitia wito wa Bring Back Our Girls limesema kupitia ukurasa wake wa facebook kuwa linalo furaha sana na linashukuru hatua hiyo, na kwamba linasubiri majina ya wasichana ambao wameachiliwa.

Profesa Hauwa Biu ambaye ni mwanaharakati mwanamke eneo la Maiduguri amesema "tunashukuru serikali ya Nigeria, na kama Oliver Twist, tunaomba zaidi.

Mwaka jana mazungumzo yalivunjika pale Boko Haram lilipotaka dola bilioni 5.2 kama fidia. Hata hivyo haijabainika ikiwa kulikuwa na malipo yoyote kwa kuachiliwa kwa wasichana 21.

Wasichana 276 walitekwa nyara Aprili mwaka 2014 wakiwa shuleni eneo la Chibok. Juhudi za serikali kuwanusuru ziliambulia patupu, hali iliyozua ghadhabu za kimataifa. Baadhi ya wasichana hao wakitoroka kivyao, lakini wengine wamesalia mikononi mwa kundi hilo lenye itikadi kali za kidini.

Mwezi Mei mwaka huu, msichana Amina Ali Nkeki alifaulu kutoroka kutoka mikononi mwa kundi hilo, na alisema kuwa baadhi ya wenzake wameaga dunia kutokana na maradhi na wengine wameolewa na wapiganaji, huku wengine wakiwa wajawazito au wanalea watoto waliowazaa.

Mji wa Borno katika eneo la Maiduguri ndio chimbuko la kundi la Boko Haram, ambapo kwa kipindi cha miaka 7 iliyopita, kundi hilo limewaua maelfu ya watu na kulazimisha zaidi ya watu milioni 2 kuyahama makwao, huku wengine wakitekwa nyara na kujeruhiwa.

Tangu wakati huo, Nkeki amekuwa akihifadhiwa na idara ya ujasusi ambapo pia anapata matibabu na ushauri nasaha. Hata hivyo serikali imelaumiwa kwa kumtenga msichana huku wanaharakati wakiuliza ikiwa amefanywa mzuiliwa wa serikali.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE

Mhariri: yusuf saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW