Boko Haram wachinja 56 Nigeria
31 Agosti 2015Gavana wa jimbo hilo la Borno Kashima Shetima alithibitisha shambulizi dhidi ya kijiji cha Baanu wakati alipofanya mkutano na wazazi wa wanafunzi 219 wa kike waliochukuliwa mateka na Boko Haram kutoka shuleni mwaka uliopita. Alhamisi wiki iliyopita, zilitimia siku 500 tangu wasichana hao walipotekwa mjini Chibok.
Shetima alisema mgogoro wa Boko Haram umegeuka janga kwa Nigeria, kwa sababu waasi hao hawachaguwi dini, na wala hawana huruma ya kikabila, na kuongeza kuwa siku ya Jumamosi waliuwa watu 56 katika kijiji hicho kilichoko katika mtaa wa Nganzai.
Shetima alisema wakati akizungumza na wazazi hao, miili ya wahanga wa shambulizi hilo la Boko haram ilikuwa bado imezagaa katika mita ya kijiji hicho, kwa sababu karibu kila mkaazi alikuwa amekimbia kuokoa maisha yake. Lakini gavana huyo hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusu shambulizi hilo.
Mashambulizi yazidi makali
Wakazi wa Baanu waliokuwa wanakimbia walisema walivamiwa na Boko Haram usiku wa Ijumaa. Mustapha Alibe, mkulima kutoka kijijini hapo, alisema waliporejea kijijini asubuhi baada ya kukaa porini usiku mzima, waliona miili ikiwa imetapakaa mitaani.
Uasi wa Boko Haram uliodumu kwa miaka sita sasa, umesababisha vifo vya karibu watu elfu 20, huku watu wasiopungua alfu moja wakiwa wameuawa na wapiganaji hao tangu kuchaguliwa kwa rais Muhammadu Buhari mwezi Machi, akiahidi kulisambaratisha kundi hilo.
Wanajeshi wa Nigeria kwa kushirikiana na wa Chad wamewafurusha Boko Haram kutoka miji 25 waliyokuwa wanaishikilia kwa miezi kadhaa katika eneo lililotangazwa na Boko Haram kuwa dola ya Kiislamu au Khilafa.
Tangu wakati huo waasi hao ambao mwezi Machi walitangaza utiifu kwa kundi la dola la Kiislamu IS, walianza kutumia mbinu za kushambulia na kukimbia pamoja na miripuko ya kujitoa muhanga, hasa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi.
Waenea maeneo mengine ya nchi
Katika tukio tofauti, maafisa wa serikali wameripoti kuwapo na ongezeko la mawakala wa Boko Haram mkoani Lagos na maeneo mengine ya Nigeria, nje ya eneo kuu la harakati za kundi hilo kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Msemaji wa idara ya ujasusi ya Nigeria Tony Opuiyo, alisema katika taarifa kuwa Boko Haram wanajaribu kutanua harakati zao baada ya kufurushwa katika maeneo ya mijini kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
Mashirika ya usalama yamewakamata washukiwa 14 wa Boko Haram mjini Lagos, katika mji mkuu Abuja na maeneo mengine ya nchi nje ya ukanda wa kaskazini-mashariki katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, alisema Opuiyo.
Waliokamatwa ni pamoja na viongozi wa magenge, ambao baadhi walikiri kuhusika katika mashambulizi ya karibuni ya kujitoa muhanga. Serikali ilisema siku ya Ijumaa kuwa walimkamata kijana mdogo aliekuwa anauchunguza uwanja wa kimataifa wa ndege wa Abuja kwa niaba ya Boko Haram.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape
Mhariri: Daniel Gakuba