Boko Haram waendeleza mashambulizi kaskazini mwa Nigeria
13 Machi 2015Mshambuliaji wa kike wa kujitoa muhanga alijiripua hapo jana katika soko la Monday ambalo limeshambuliwa mara kadhaa na waasi wa Boko Haram likiwemo shambulizi la siku ya Jumamosi iliyopita.
Mkuu wa polisi wa jimbo la Borno Clement Adoda amewaambia wanahabari kuwa kiasi ya watu saba wameuawa na wengine kumi na saba kujeruhiwa katika shambulizi hilo.
Duru zinaarifu kuwa wahudumu wa afya wanalemewa kwani walikuwa bado wanawatibu majeruhi 139 wa mashambulizi ya Jumamosi wakati majeruhi zaidi walipofikiswha hospitalini hapo jana. Wakati huo huo Boko Haram pia imewaua kiasi ya watu kumi katika kijiji cha Ngamdu kinachoiunganisha miji ya Maiduguri na Damaturu.
Serikali yasema Boko Haram inatapatapa
Shambulizi hilo la hivi punde linakuja huku serikali ya Nigeria ikilitaja tangazo la Boko Haram kuwa litakuwa tiifu kwa kundi la dola la kiislamu IS kama ishara ya udhaifu kutokana na mbinyo kutoka kwa jeshi la Nigeria na washirika wake.
Msemaji wa shirika la kitaifa la usalama wa taifa Mike Omeri amesema ni kitendo cha kundi linalotapatapa na inakuja wakati waasi hao wanakabiliwa vilivyo na wanajeshi na kuongeza Boko Haram iko njiani kutokomezwa.
Omeri amesema hakuna dola la kiislamu litaruhusiwa nchini Nigeria na dola pekee litalokuwepo nchini humo ni serikali kuu ya Nigeria.
Wachambuzi wa masuala ya kiusalama wamesema tangazo la kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau kuwa kundi lake litakuwa tiifu kwa kundi la Abu Bakr al Baghdadi huenda ni mbinu ya kueneza propaganda lakini pia huenda makundi hayo mawili yakawa na mafungamano ya karibu zaidi katika siku za usoni.
Majeshi ya Nigeria, Chad , Niger na Cameroon yamekuwa yakipambana vikali na waasi hao katika kampeini kabambe ya kutaka kuwatokomeza kutoka ngome zao katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Wanajeshi wamesema wamepiga hatua katika wiki za hivi karibuni katika azma yao ya kuhakikisha eneo hilo la kaskazini mashariki liko salama kwa muda ufao ili uchaguzi mkuu nchini Nigeria unaotarajiwa tarehe 28 mwezi huu uweze kufanyika.
Operesheni za kijeshi zapamba moto
Jeshi la Nigeria limesema limetibua shambulizi la Boko Haram katika mji wa Gombi ulioko katika jimbo la Adamawa na kukamata silaha nzito.Hiyo inafuatia operesheni ya kijeshi kutoka kwa jeshi la Chad na la Nigeria la kutaka kuudhibiti mji wa Damasak katika jimbo la Borno iliyofanywa siku ya Jumatatu.
Niger imesema wamewapoteza askari na wanajeshi 24 pamoja na raia mmoja tangu nchi hiyo ilipojihusisha katika operesheni ya kukabiliana na Boko Haram.
Kiasi ya wapiganaji 513 wa Boko Haram pia wameuawa katika mapigano kusini mashariki mwa Niger kulingana na takwimu zilizokusanywa mpaka tarehe nane mwezi huu.
Shekau ameapa kuutatiza uchaguzi mkuu nchiniNigeria. Tangu Boko Haram ianzishe uasi mwaka 2009, kiasi ya watu 13,000 wamuawa na wengine takriban milioni moja na laki tano wameachwa bila ya makaazi.
Hapo jana kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundi ilionya kuwa hali inazidi kuzorota kwa walioachwa bila ya makaazi waliotorokea katika eneo la ziwa Chad.
Mwandishi:Caro Robi/Afp/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu