1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram wapanga kushambulia Abuja

Sekione Kitojo
13 Mei 2017

Mtu ambaye anafikiriwa kuwa mpiganaji wa kundi la Boko Haram amesema kundi hilo la wanamgambo wenye itikadi kali linapanga kushambulia kwa mabomu mji mkuu wa Nigeria, Abuja, katika vidio iliyopatikana na Reuters.

Nigeria Boko Haram - Kinder als Selbstmordattentäter
Moja ya mashambulio ya kundi la Boko Haram nchini NigeriaPicha: picture-alliancce/AP Photo/S. Maikatanga

"Mashambulizi  zaidi  ya  mabomu  yanakuja, ikiwa  ni  pamoja  na  Abuja  ambako  mnahisi mko  salama," amesema  mtu  huyo  katika  vidio ambayo  imepatikana na  waandishi  habari wa  Sahara, tovuti ya  waandishi  habari  yenye  makao  yake  nchini  Marekani, na mwandishi  habari  wa  Nigeria Ahmad Salkida.

Reuters  hata  hivyo  hawakuweza  kuthibitisha  uhalali  wa  vidio  hiyo.

Msikiti mjini Maiduguri ambao umeshambuliwa na wanamgambo wa Boko HaramPicha: picture-alliancce/AP Photo/J. Ola

Idara ya  usalama  wa  taifa  nchini  Nigeria , DSS , mwezi  Aprili  ilisema  imezuwia  mipango ya   wanamgambo  wa  Boko Haram  wenye  mafungamano  na  kundi  la  Dola  la  Kiislamu kushambulia  balozi  za  Uingereza  na  Marekani mjini  Abuja.

Kiasi  ya  wasichana 82 waliachiwa  huru Jumamosi  iliyopita  kwa  kubadilishana  na makamanda  wa  kundi  la  Boko  Haram  baada  ya  kushikiliwa  kwa  muda  wa  miaka mitatu. Walikuwa  ni  miongoni  mwa  kiasi  wasichana  270  waliokamatwa  na  kundi  hilo  la jihadi  kutoka  mji  wa  Chibok  kaskazini  mashariki  mwa  Nigeria  mwezi  Aprili  mwaka 2014.

Katika  vidio ya  pili  iliyopatikana  na  Reuters , mmoja  kati  ya kundi  la  wanawake wanne waliojifunika  nyuso  zao  alidai  kuwa  miongoni  mwa  wasichana  waliotekwa  na  hataki kurejea  nyumbani.

Baadhi ya wasichana walioachwa huru na kundi la Boko Haram mwaka 2016Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Aghaeze/

"Hatutaki  kurudi  kuungana  na  wazazi  wetu kwasababu  hawamuabudu Allah , na nawaomba  kujiunga  nasi," alisema, akishikilia  bunduki  na  akizungumza  kwa  lugha  ya Kihausa ambayo  huzungumzwa  na  watu  wa  kaskazini  mwa  Nigeria. Aliongeza : "Hatukuolewa  kwa  kushurutishwa  na  mtu  yeyote. "Ndoa ni utashi  wa  mtu."

Reuters  haikuweza  kuthibitisha uhalisia  wa  vidio  hiyo.

Mpatanishi  na  mwanasheria  Zannah Mustapha  amesema  baadhi  ya  wasichana waliotekwa walikataa  kuachiliwa  huru , na  kuzusha  hofu kwamba  wamepata itikadi  kali  ya wapiganaji  hao  wa  jihadi, na  huenda  wanajisikia  woga ama aibu  kurejea  katika  maisha yao  ya  zamani.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri : Yusra Buwayhid