Tinubu apendekeza miezi 9 ya mpito Niger
1 Septemba 2023Tinubu ametoa pendekezo hilo akirejea kile kilichowahi kutokea Nigeria ambayo ililazimika kuingia kwenye kipindi cha mpito mwishoni mwa miaka ya 1990 baada ya mapinduzi.
Rais Bola Tinubu ametoa pendekezo hilo akisema kuwa, Nigeria ilirejea kwenye utawala wa kiraia mwaka 1999 baada ya kipindi cha mpito cha miezi tisa kilichoanzishwa na kiongozi wa zamani wa kijeshi Jenerali Abdulsalami Abubakar, ambaye pia ameongoza wajumbe kukutana na viongozi wa kijeshi wa Niger.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Tinubu imesema kuwa kiongozi huyo haoni ni kwanini hatua hiyo haiwezi kuigwa na Niger ikiwa mamlaka za kijeshi zinazotawala nchini humo zina nia njema. Licha ya pendekezo hilo, taarifa ya Rais Tinubu imesema kuwa Niger haitapewa nafuu ya vikwazo ilivyowekewa na Jumuiya ya ECOWAS ambapo yeye ni mwenyekitii hadi utawala wa kijeshi wa taifa hilo utakapofanya marekebisho chanya.
Awali, Algeria ambayo ni jirani wa Niger ilipendekeza kipindi cha mpito cha miezi sita kwa viongozi wa Jumuiya ya kikanda ya Afrika ya magharibi, ECOWAS katika juhudi za kuepusha Jumuiya hiyo kuingilia kati kijeshi Niger.
Jumuiya hiyo ya ECOWAS imeiwekea vikwazo Niger baada ya wanajeshi kumng'oa madarakani Rais Mohamed Bazoum katika mapinduzi ya Julai 26. Awali Jumuiya hiyo ya kuchumi ya Afrika ya magharibi ilitishia kuingilia kati kijeshi nchi hiyo kama isingerejesha utawala wa kiraia.
Soma zaidi: ECOWAS yakataa kipindi cha mpito cha miaka mitatu Niger
Katika kauli iliyotolewa Alhamisi, Jumuiya hiyo ilisisitiza kuwa inataka Bazoum arejeshwe madarakani kwa njia inayofaa.
Utawala mpya wa kijeshi wa Niger wenyewe umesema kuwa unahitaji walau miaka mitatu ya kipindi cha mpito ili kurejesha utawala wa kikatiba na wameliamuru jeshi la polisi nchini humo kumuondoa katika taifa hilo balozi wa Ufaransa. Utawala huo kupitia barua ulioiandikia wizara ya masuala ya kigeni ya Ufaransa umeamuru pia balozi huyo aondolewe kinga ya kidiplomasia.
Itakumbukwa kuwa jana Alhamisi, wizara ya mambo ya ndani ya Niger ilitangaza kuyasimamisha mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kimataifa kuendesha shughuli katika maeneo kunakofanyika operesheni za kijeshi. Hata hivyo haikusema ni maeneo gani hasa yaliyoguswa na tangazo hilo lakini ilieleza kwamba hatua hiyo inatokana na hali ya sasa ya kiusalama.
Mapinduzi ya kijeshi nchini humo yamezua wasiwasi miongoni mwa mataifa ya Afrika ya Magharibi. Hofu ya mapinduzi zaidi imeongezeka baada jeshi kumpindua rais wa Gabon, Ali Bongo muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa hivi karibuni, uliokuwa umegubikwa na utata.
Chanzo: APE