1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUjerumani

Balozi wa Ujerumani mjini Moscow aitishwa kujieleza

Saleh Mwanamilongo
4 Machi 2024

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilimwita Jumatatu balozi wa Ujerumani mjini Moscow kufuatia kuvujishwa kwa nyaraka za siri za jeshi la Ujerumani kuhusu Ukraine.

Balozi wa Ujerumani nchini Urusi Alexander Lambsdorff aitishwa kwenye wizara ya mambo ya nje Moscow
Balozi wa Ujerumani nchini Urusi Alexander Lambsdorff aitishwa kwenye wizara ya mambo ya nje MoscowPicha: Prokofyev/TASS/picture alliance Vyacheslav

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi, la RIA Novosti, liliripoti leo kwamba balozi wa Ujerumani alifika katika wizara ya mambo ya nje ya Urusi mjini Moscow, ambapo aliitwa kuhusiana na mazungumzo yaliyovujishwa ya maafisa wa Ujerumani kuhusu vita nchini Ukraine.

Taarifa hiyo imesema kuwa Balozi Alexander Graf Lambsdorff aliwasili katika wizara hiyo Jumatatu asubuhi, bila kutoa maoni yoyote kwa waandishi wa habari. Rekodi ya sauti ya dakika 38 ya mazungumzo kati ya maafisa wa jeshi la Ujerumani ilichapishwa jioni ya Ijumaa kwenye mitandao ya kijamii ya Urusi.

Urusi yazituhumu nchi za Magharibi

Maafisa hao walikuwa wakijadili uwezekano wa kutumwa nchini Ukraine kwa makombora ya Taurus yaliyotengenezwa Ujerumani na athari zake. Na mada nyingine zilizojadiliwa na maafisa hao wa ujerumani ni pamoja na kulenga makombora kwenye daraja muhimu juu ya mlango wa bahari wa Kerch unaounganisha Urusi na Crimea, jimbo ambalo lilitwaliwa na Urusi mnamo 2014.

Serikali ya Urusi imesema leo Jumatatu kwamba nyaraka hizo za siri zilizovujishwa zinaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi katika mzozo wa Ukraine. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema haikuwa wazi kama jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, walikuwa wanachukua hatua kama mpango wao wenyewe au ilikuwa ni sehemu ya sera ya serikali.

''Ni juu ya kudhoofisha umoja wetu''

Waziri wa ulinzi wa Ujeumani Boris Pistorius (Kulia ) asema Urusi inalenga kupotosha habari Picha: Klaus-Dietmar Gabbert/dpa/picture alliance

Serikali ya Berlin siku ya Jumapili iliishutumu Urusi kwa kujaribu "kuyumbisha" Ujerumani kwa kuchapisha rekodi ya sauti ya mazungumzo ya siri ya maafisa wake wa jeshi kwenye mitandao ya kijamii ya Urusi. Wazirí wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amesema Putin analenga kuudhofisha umoja wa Wajerumani.

"Tukio hilo ni wazi zaidi ya kunaswa na kuchapishwa kwa mazungumzo ndani ya jeshi la anga. Ni sehemu ya vita vya habari ambavyo Putin anaendesha. Hakuna shaka juu ya hilo. Ni shambulio la mseto linalolenga kupotosha habari. Ni kuhusu mgawanyiko, ni juu ya kudhoofisha umoja wetu.'', alisema Pistorius.

Miito ya uchunguzi wa ndani

Hata hivyo, wanasiasa wa upinzani nchini Ujerumani Jumapili walipendekeza uchunguzi ufanyike bungeni, ikiwa ni pamoja na maswali kwa Kansela Olaf Scholz.

Jana Jumapili, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa wito kwa ulimwengu kuisaidia Kyiv kushinda kile alichokiita "maovu ya Urusi". Kauli hiyo ilitolewa na Zelensky baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Urusi katika jimbo la Odesa lililosababisha vifo vya watu12, wakiwemo watoto watano.

Vyanzo: AFP, Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW