1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Bolsonaro apinga matokeo ya uchaguzi

23 Novemba 2022

Miezi zaidi ya mitatu baada ya kushindwa uchaguzi, Rais Jair Bolsonaro wa Brazil ametowa tuhuma nzito dhidi ya mfumo wa kielektroniki akiitaka mahakama inayoshughulikia uchaguzi kuyafuta kabisa matokeo yake.

Brasilien | Pressestatement von Jair Bolsonaro nach der Wahl
Picha: Andressa Anholete/Getty Images

Wakili wa Bolsonaro aliyeandika ombi la kurasa 33 kwa niaba ya mteja wake na chama chake cha Liberal Party, Marcelo de Bessa, alisema siku ya Jumatano (23 Novemba) ikiwa hatua aliyotaka rais huyo ingechukuliwa, ingeliweza kumpa asilimia 51 ya kura halali zilizosalia.

Kiongozi wa chama chake, Valdemar Costa, na mkaguzi wa mahesabu aliyekodiwa na chama hicho waliwaambia waandishi wa habari kwamba uchunguzi wao "uligunduwa kuwa mashine takirbani 280,000, ambazo ni asilimia 59 ya mashine zote zilizotumika kupigia kura tarehe 30 Oktoba, hazikuwa na sehemu ya nambari ya kitambulisho."

Ingawa hakuna hata mmoja aliyeeleza jinsi hilo lilivyoathiri matokeo ya uchaguzi wenyewe, lakini walisema wanaitaka mahakama ya uchaguzi kuzifuta kura zote zilizopigwa kwenye mashine hizo.

Hati ya malalamiko imeelezea mapungufu hayo kwamba hayarekebishiki na kwa hivyo yanatilia shaka uhalali wa matokeo yote ya uchaguzi.

Jaji wa Mahakama ya Uchaguzi apinga

Muda mchache baada ya chama cha Bolsonaro kutoa tamko lake, mkuu wa mahakama ya uchaguzi alisema  "hakuna uwezekano wowote kuwa chama hicho kingeliathirika na changamoto hiyo iliyotokea.

Rais wa Mahakama ya Juu ya Uchaguzi ya Brazil, Alexandre de Morae.Picha: Evaristo Sa/AFP

Alexandre de Moraes alisema mahakama isingelitazingatia malalamiko kama hayo hadi pale chama hicho kitakapotowa ripoti ndani ya masaa 24 ambayo itajumuisha matokeo kutoka uchaguzi wa kwanza wa tarehe 2 Oktoba.

Katika uchaguzi huo, chama cha Bolsonaro kilipata viti zaidi kwenye mabaraza yote mawili ya bunge kuliko chama chengine. 

Mmoja wa wachambuzi mashuhuri wa siasa nchini Brazil, Cremor de Souza, alisema maneno ya de Moraes "yanaashiria kwamba mahakama inayohusika na uchaguzi ina uwezekano mkubwa wa kukataa ombi hilo."

Athari kwa matokeo ya uchaguzi

Rais mteule wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva.Picha: Carl De Souza/AFP

Tatizo linalotajwa kwenye malalamiko ya Bolsonaro na chama chake hayakuwahi kufahamika kabla.

Hata hivyo, wataalamu walisema hayaathiri matokeo, kwa kuwa kila mashine inaweza kutambuliwa kirahisi kwa njia nyengine, kama vile mji ama wilaya kura ilikopigwa.

Vile vile, ingawa mashine hazikuwa na nambari za vitambulisho vya wapigakura, nambari hizo zinaonekana kwenye kipande cha kupigia kura. 

Msimamo huu wa Bolsonaro umetangazwa wakati tayari mahakama ya uchaguzi ilishatangaza ushindi wa hasimu wake, Luiz Inacio Lula da Silva, na hata washirika wengi wa rais huyo wameshayakubali matokeo hayo. 

Hata hivyo, waandamanaji kwenye miji kadhaa ya nchi hiyo wamekataa kuyakubali matokeo, hasa baada ya Bolsonaro mwenyewe kukataa kukiri kushindwa tangu mwanzoni.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW